Nairobi. Katika hali ya kushangaza, uchunguzi (autopsy) uliofanywa kwa miili 110 ya waliokuwa waumini wa Kanisa la Good News International linaloendesha shughuli zake katika Msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi nchini Kenya, umebaini kuwa, baadhi ya waathiriwa waliuawa kwa kukosa hewa na kunyongwa.
Zoezi la uchunguzi huo lilifanyika katika chumba cha hifadhi ya maiti cha Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Malindi, lililoongozwa na Mwanapatholojia Mkuu wa Serikali Johansen Odor na kubaini viashiria kwa watoto wawili walifariki kwa kukosa hewa kutokana na kuzibwa mdomo na pua.
Kwa mujibu wa mtandao wa gazeti la Nation uliomnukuu Mwanapatholojia huyo, katika zoezi hilo la uchunguzi lililofanyika jana Mei 2, mwaka huu timu hiyo ilifanikiwa kuchunguza miili ya watoto tisa wenye umri kati ya mwaka mmoja na nusu hadi kumi na mwanamke mmoja.
"Kwa ujumla walikuwa na sifa za njaa...Lakini miili miwili ya watoto ilikuwa na sainosisi (cyanosis), au kubadilika rangi ya kibluu kwenye kucha ... kulikosababishwa na kukosa hewa. Hii inamaanisha kuwa walinyimwa oksijeni wakati wa kifo," Odor alisema wakati wa mkutano na wanahabari.
Hii inamaanisha kuwa kwa matokeo hayo, ni wazi kabisa kuna viashiaria vya mauaji, hasa ya watoto, ambao kimsingi ndiyo wengi katika wahanga wa shughuli za ibada zilizokuwa zikiongozwa na mhubiri Mackenzie ambaye baadaye leo, anatarajiwa kufikishwa mahakamani.
Awali kwa mujibu wa Mwanapatholojia Odor, zoezi hilo lilikuwa na changamoto kiasi cha kulazimika kuweka mashine za X-ray kwa ajili ya kukadiria umri.
"Miili yote ilikuwa na sifa za njaa. Tuliona hakuna chakula tumboni kwani safu ya mafuta ilikuwa ndogo sana. Ini lilikuwa na mafuta, dalili ya njaa," Odor amesema.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa viungo vyote vya mwili vilikuwa shwari lakini viwango vya kuoza vilifanya iwe vigumu kutaja wakati sahihi ambapo waathiriwa walikufa njaa au kuuawa.
Familia zilizo na jamaa waliopotea au waliokufa pia zitakusanywa DNA zao kuanzia leo kwa ajili ya kulinganisha.
Awali, Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya Kithure Kindiki alibainisha kuwa serikali itaunda tume ya uchunguzi juu ya vifo hivyo vya kundi la Shakahola na kupendekeza hatua zitakazochuliwa dhidi ya maafisa wa umma ambao watapatikana na hatia ya uzembe kazini.
Kindiki alisema timu hiyo itachunguza vifo hivyo na kupendekeza hatua za uwajibikaji.
"Tume ya uchunguzi itapendekeza hatua zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya afisa yeyote wa umma ambaye alizembea, alishindwa kuchukua hatua au uzembe wa aina yeyote uliosababisha vifo vya watu wetu,” amesema.
Kindiki ameongeza kuwa hakuna miili zaidi itakayofukuliwa kutokana na hali hewa kuwa mbaya, huku lengo likigeukia sas katika kutambua wa mabaki ya miili 110 ambayo ilifukuliwa mwezi uliopita.
"Ufukuaji wa kaburi umesitishwa kwa sasa kwa sababu ya mvua kubwa na utaanza tena wakati ambapo itabainika kuwa salama kufanya hivyo. Hatutaki kuingilia ushahidi wa sampuli na eneo," amesema na kuongeza kuwa eneo hilo, bado chini ya ulinzi wa polisi.
"Baada ya siku mbili, tutapeleka helikopta kufanya uchunguzi wa angani na tunasubiri masuala machache ya uendeshaji kutatuliwa."
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Upelelezi katika Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Abdallah Komesha, amepekwa kuongoza timu inayochunguza vifo vya watu wengi vilivyotokea katika msitu huo wa Shakahola.
Kufikia Jumanne wiki iliyopita, watu 461 walikuwa wameripotiwa kupotea na familia na marafiki.
"Hatuna uhakika wote wanahusishwa na tukio la Shakahola," Waziri Kidiki amesema. Na kwamba uchunguzi wa fifo hivyo unatarajiwa kuchukua muda huku Mwanapatholojia Oduor akiweka wazi kuwa kazi ya kulinganisha sampuli za DNA kwa waathiriwa na jamaa zao, inaweza kuchukua mwezi mmoja au zaidi.