WATU wanne wakiwamo waendesha bodaboda watatu wanaokadiliwa kuwa na umri wa kati ya miaka 26 na 30 wameuawa kikatili kwa kushambuliwa na kuchomwa sehemu mbalimbali za miili yao kisha pikipiki zao kutelekezwa...
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi (CP), Awadhi Juma.
...katika vichaka nje kidogo na Kijiji cha Nyakiswa, Kata ya Kyanyari wilayani Butiama mkoani Mara.
Shambulio hilo inaelezwa kufanyika na wahalifu ambao bado hawajafahamika na lengo lao halikufahamika kwa haraka usiku wa kuamkia Mei 28, majira ya saa tano usiku huku wakitokomea kusikojulikana na kutelekeza pikipiki tatu walizokuwa nazo waendesha bodaboda hao.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana baada ya kufika katika eneo la tukio, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo ya Jeshi la Polisi (CP), Awadhi Juma, alisema uchunguzi umeanza kufanyika na hakuna mtu yeyote aliyekamatwa kutokana na tukio hilo kufanyika nyakati za usiku.
Aidha, alisema watu walioshambuliwa na kuuawa ni wanne ambao wote ni wanamume bila kuwataja majina na kueleza kuwa kati yao watatu wametambuliwa kuwa ni waendesha bodaboda katika eneo la Kijiji cha Nyakiswa, lakini mmoja bado hajatambulika.
Akifafanua kuwa watu hao ni wahalifu na kuwa dhumuni lao bado halijafahamika kutokana na pikipiki walizokuwa nazo waendesha bodaboda hao kutokuchukuliwa na kukutwa katika eneo la tukio.
“Watu hawa wanaonekana walishambuliana kwa muda mrefu kutokana na eneo husika kukutwa na dalili za purukushani ndipo waendesha bodaboda hao walipo zidiwa kwa kuchomwa na vitu vyenye ncha kali vinavyosadikiwa kuwa silaha za jadi hadi kuwasababishia mauti,” alisema CP Awadhi.
Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Rodovick Kahegele, akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu alikemea vikali vitendo vya namna hiyo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuwabaini wahusika ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Katika kipindi cha mwezi Mei, zaidi ya matukio manne ya mauaji ya kutumia silaha za moto pamoja na jadi yametokea katika maeneo mbalimbali mkoani Mara hali iliyosababisha Jeshi la Polisi nchini kutuma kikosi maalum cha operesheni kikiongozwa na CP Awadhi katika mikoa ya kipolisi Mara na Tarime Rorya, kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kusaka wahalifu ambao wamekuwa wakitekeleza matukio hayo.
Aidha, alisema kikosi hicho kimefanikiwa kuwakamata watuhumiwa sugu 21 wa uhalifu wakiwamo waliofanya mauaji ya mfanyabiashara wa madini mkoani humo, daktari Isack Daniel yaliyotokea Mei 3, mwaka huu.