YANGA inakutana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwenye mechi ya Nusu fainali ya Shirikisho Mei 10, ngoma ikianzia Jijini Dar es Salaam. Hizi dondoo za Marumo;
UKATA
Timu hiyo inakabiliwa na ukata mkubwa ambapo imekuwa ikihaha kujiendesha kwenye ligi ya ndani na hata kimataifa ingawa pia imekuwa na mashabiki wachache. Viongozi wao wawili walikuwa wameshikiliwa nchini Libya hivikaribuni kwa kushindwa kulipa bili za hoteli na gharama zingine walipokwenda kucheza na Al Khdar mpaka Serikali ilipoingilia kati.
DYLAN KERR
Kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerr amepewa Ukocha wa muda kwenye klabu hiyo tangu Januari baada ya mambo kuwa mabaya. Kerr aliithibitishia Mwanaspoti jana kwamba ndiye anayeongoza jahazi hilo kwa muda.
MKIANI LAKINI BALAA
Marumo ipo nafasi mbili kutoka mkiani mwa Ligi Kuu ya Afrika Kusini, ikiwa imesaliwa na mechi tatu kumaliza msimu kwa kujinusuru kushuka Daraja. Imeshinda mechi tano tu kati ya 27 walizocheza.
UZITO MWEPESI
Kwa mujibu wa wachambuzi wa Afrika Kusini, asilimia kubwa ya wachezaji wa timu hiyo ni wa daraja la kawaida ambao hawawezi kupata namba kwenye timu zenye uwezo wa kiuchumi nchini humo.
KIMATAIFA WAPO
Sapraizi ya kipekee kwa wachezaji wa klabu hiyo kwa mashabiki ni kwamba, kimataifa msimu huu wameshinda mechi nane, sare moja kati ya michezo 12 waliyocheza mpaka sasa. Kitendo cha kutoa matajiri wa Pyramids kiliduwaza wengi.
KUNDINI
Ilianzia raundi ya pili kwenye Shirikisho. Iliongoza Kundi A la michuano hiyo kwa pointi 12. Ilikuwa pamoja na USM Alger ya Algeria(Algeria), FC Lupopo(DR Congo) na Alkhdar(Libya).
RANGA
Ranga Chivaviro ndiye staa wao, amefungana na Fiston Mayele wa Yanga kwenye msimamo wa wafungaji wa Shirikisho msimu huu baada ya mechi za juzi. Ranga anahusishwa na timu kibao za Afrika Kusini na muda wowote huenda akang’oka kwenye klabu hiyo.