Wafanyabishara: Mfumo wa kodi ufumuliwe tupumue



Dar es Salaam. Wakati kodi ya forodha inayotozwa kwa mizigo inayoingia nchini ikiwa ni moja ya kilio kikuu cha wafanyabiashara wa soko la Kariakoo mapendekezo ya kufumuliwa kwa mfumo wa kodi yameibuka.

Kufumuliwa kwa mfumo wa kodi kunatajwa kuwa mwarobaini wa matatizo mengi yanayolalamikiwa na wafanyabiashara hao.

Hayo yamesemwa katika mkutano wa wafanyabiashara na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa unaofanyika katika viwanja cya Mnazi Mmoja huku ukiwahusisha pia mawaziri mbalimbali akiwemo  wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba.

Kufanyika kwa mkutano huu ni matokeo ya mgomo ambao umedumu kwa siku tatu sasa wakati wafanyabiashara hao wakishinikiza serikali iwasikilize na kutatua kero zao kwa uwazi.


Akizungumza katika mkutano huo, Wajibu Mpandila ambaye ni mfanyabiashara amesema mioyo ya wafanyabiashara wengi inavuja damu kwa sababu mifumo ya kodi bandarini si rafiki hasa ule wa forodha.

Hiyo ni kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kutosomana kwa mifumo wa forodha na mfumo wa utoaji risiti.

"Fumua mfumo wa Kodi bandarini ili watu waweze kupona, ujio wa EFD haikubadili mifumo ya kodi iliyokuwapo bandarini hii ndiyo inafanya kuwepo kwa mianya ya mazungumzo kati ya wafanyabiashara na watu wa TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania)," amesema


Amesema suala hilo limekuwa likiwafanya watu wanaosoma vyuoni kudai kuwa wanasomea TRA na kusahau kile wanachokisomea kwa sababu wanaamini wakifika kazini watapata fedha nyingi.

Amesema ifike wakati kama nchi iwe na mifumo ya kodi ya wazi na elekezi kwa kile alichokieleza kuwa mifumo iliyopo sokoni na bandarini haviendani.

"Mimi naamini mapinduzi haya yanaweza kuleta historia lakini tukiweka danadana hatutatoka, shida itaendelea kuwa palepale kwa sababu mifumo ya kodi bandarini inawatia majaribuni watu wa TRA,"

Mfanyabiashara mwingine ambaye hakutaja jina lake alisema licha ya kuwa na moyo wa kufanya biashara ila wamekuwa wakikatishaa tamaa.

"Tufanye mabadiliko makubwa ili tuweze kwenda mbele tunaumizwa sana, Viongozi wetu hawashuki chini wanajifungia ndani,"

Kwa upande wake Irab Nyenge mfanyabiashara anayefanya shughuli zake Dar es Salaam, Kigoma na Burundi amesema amekuwa akisumbuliwa licha ya kufuata taratibu zote.

"Kuna vijana wadogo wanachukua mzigo wako wanakuomba TIN namba (Namba ya mlipa kodi) ukiwapa wanasema haisomi wakati TIN namba yako umeshawaambia ni ya nje ya nchi (Burundi). Kila mfanyabiashara anaposafirisha mizigo lazima atafutiwe sababu ili aombwe rushwa,”amesema.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad