Dar es Salaam. Wakati wafanyabiashara wakiendelea na mgomo katika Soko la Kariakoo, hoja imeibuka kuhusiana na mashine za EFDs; huku wakiona maombi ya serikali kusitisha mgomo, hayajibu kero zao.
Moja ya kijiwe kilichongozwa na mfanyabiashara maarufu ‘Kipara’ ambaye amewaeleza wenzake kwamba kauli ya Majaliwa kwamba wafungue biashara na kero zao zitakwenda kutatuliwa, ni nyepesi ambayo wakiitekeleza ni kukubali kuumizwa.
Kipara akiwa kama kiongozi wa mjadala huo alihoji: "Kwanini Rais Samia yeye mwenyewe asije, viongozi wetu hawewezi kutuambia tusitishe mgomo wakati wenyewe tumepima kilichozungumzwa, na tumeona mambo ni yale yale. Kweli unatuletea hoja nyepesi kwenye biashara zetu! Hizi mashine za EFDs zinaonyesha mauzo tu na haionyeshi matumizi, sisi kwetu hilo ni tatizo," amehoji.
Kauli ambayo hiyo ilipokelewa kwa makofi na wafanyabiashara wenzake, iliibua hoja nyingine kwamba mashine za EFDs ni tatizo; jambo ambalo linachangia kwa wafanyabiashara hao, kutotoa risiti kama inavyodaiwa na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).
Kwa kuwa wafanyabiashara wamekuwa wakichukuliwa hatua wanapobainika kutotoa risiti za kielektroniki, wanadhani hiyo ni sheria kandamizi na kwamba mtu pekee kunusuru hilo ni Rais Samia Suluhu Hassan.
Japo inasadikika kuwa Waziri Mkuu ataonana na wafanyabiashara hao kesho, lakini wasiwasi mkubwa wa wafanyabiashara hao ni kuingiziwa siasa kwenye kero zinazowakabili.
Kwa mujibu wa TRA, kiini cha mgomo kimechangiwa na baadhi ya wafanya biashara kutokuwa waaminifu katika utoaji wa risiti.
"Wengine wanatoa risiti wengine hawatoi, wengine wanatoa risiti kwa kiasi pungufu tofauti na bei halisi, wengine risiti moja inasindikiza mizigo kutwa," amesema Mkurugenzi wa Elimu kwa mlipakodi TRA, Richard Kayombo.
Mwananchi