Na Dotto Kwilasa, DODOMA.
MIILI ya watu wanne waliokufa Kwa tuhuma za ujambazi Aprili 25,2023 majira ya saa 03:10 Jijini hapa tayari imeshatambuliwa na kufanyiwa taratibu za maziko na ndugu zao.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Kitengo cha kuhifadhi maiti(Mochwari) Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma Beda Anthony miili hiyo yote imetambuliwa na ndugu zao na kwamba wote walikuwa wenyeji wa Mkoa wa Mbeya.
Akizungumza na Jamhuri jijini hapa leo Mei 5,2023 amewataja marehemu hao kuwa ni pamoja na Godfrey Athman Mwashinga ambaye alitambuliwa Mei 1,2023 ambapo alizikwa Mailimbili-Dodoma na Baraka Lusekelo aliyetambuliwa na ndugu zake Mei 5,2023 kisha kusafirishwa Mkoani Mbeya kwa taratibu za mazishi .
Wengine ni Timothy Kabuje aliyetambuliwa Mei 1,2023 na kuzikwa Mkonze-Dodoma pamoja na Shukrani Gambi aliyetambuliwa tangu Aprili 4,2023 na kuzikwa Ntyuka Jijini hapa.
Mnamo Aprili 26,2023,Kamanda wa Jeshi la Polisi Dodoma Martine Otieno aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa Jeshi hilo limewathibiti majambazi wanne wa kiume wenye umri kati ya 25-30 waliokuwa katika harakati za kufanya tukio la unyang'anyi wa kutumia silaha nyumbani kwa Edna Joseph Kashashari (41), mfanyabiashara.
Kamanda Otieno alieleza kuwa majambazi hao walivamia nyumbani kwa Bi. Edna Joseph Kashashari (41), mfanyabiashara, mkazi wa Kisasa wakiwa wamevaa barakoa usoni na kufanikiwa kunyang'anya pesa taslim 1,100,000/= simu ya Samsung moja na simu ndogo tatu baada ya watu hao kumtishia kumkata mapanga ndipo mhanga alipiga kelele za kuomba msaada.