Bernard Kamilius Membe alizaliwa tarehe 9 Novemba, 1953, Rondo, Chiponda, katika Mkoa wa Lindi, akiwa ni mtoto wa pili kati wa watoto saba (7) waliozaliwa katika familia ya Mzee Kamillius Anthony Ntachile na Mama Cecilia John Membe. Kwa kabila, Bernard Membe ni Mmwera, na kama ilivyo desturi ya Wamwera, watoto hutumia jina la ukoo wa Mama. Hivyo watoto wote saba wa familia hii ya Mzee Kamillius wamekuwa wanatumia jina la upande wa mama yao, Cecilia, yaani Membe.
ELIMU:
1962 – 1968: Elimu ya msingi katika shule ya msingi ya Chiponda, Lindi.
1969 – 1972: Elimu ya Sekondari, (O-level) Namupa Seminary, Lindi
1973 – 1974: Kidato cha tano na sita (A-level) Itaga Seminary, Tabora
1975 – 1980: Aliajiriwa serikalini, ofisi ya rais
1981 – 1984: Alipata Shahada ya kwanza katika tasnia ya Sayansi katika maswala ya Siasa na mahusiano ya kimataifa (Bachelor Political Science and International Relations)
1985 – 1989: Aliendelea na ajira yake serikalini katika katika ofisi ya rais
1990 – 1992: Alipata Stashada ya Uchumi, Mahusiano ya Kimataifa na Sheria za Kimataifa (Masters- Economics, International Relations and International Law)
1993 – 1994: Alirudi serikalini kuendelea na kazi kama mchambuzi za mambo ya ulinzi na usalama
MAFUNZO:
Kati ya mwaka 1975 na 1976 Ndugu Bernard Membe alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Oljoro, Arusha. Hii ni kwa mujibu wa Sheria ambapo vijana wote waliohitimu kidato cha Sita walitakiwa kujiunga na mafunzo ya Jeshi kwa muda wa mwaka mmoja. Baada ya kuhitimu mafunzo hayo ya Jeshi, Ndugu Membe aliajiriwa katika Ofisi ya Rais, Utawala bora.
Mwaka 1978, Ndugu Membe alipata Mafunzo ya sheria za Jinai na usalama wa nchi, nchini Uingereza. Aidha, mwaka 1980, Ndugu Membe alipata mafunzo ya siasa, katika Chuo cha Chama cha Mapinduzi (CCM), Kivukoni, Dar es Salaam.
FAMILIA:Mwaka 1986, Ndugu Bernard Membe alifunga ndoa Takatifu na Dorcas Richard Masanche, katika Parokia ya Mtakatifu Joseph, Dar es Salaam. Ndugu Membe na mama Dorcas wamejaliwa kupata watoto watatu, Cecilia, Richard na Denis.
SIASA:
Ndugu Membe ametumikia nafasi mbalimbali ikiwemo Kamanda wa Vijana wa Mkoa wa Lindi, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa, na Katibu wa Secretariat ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa. Mwaka 2000, aliingia Bungeni baada ya kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Mtama, kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Licha ya uchanga wake bungeni, akiwa kama mbunge wa kawaida (back bencher), Bernard Membe alikuwa mchangiaji mkubwa wa mijadala inayohusu Amani, Ulinzi na Usalama pamoja na Utawala Bora.
Mwaka 2005, Bernard Membe alichaguliwa tena na wananchi wa Jimbo la Mtama kuwawakilisha katika Bunge la Jamhuri ya Muungano. Tofauti na kipindi cha nyuma, Bernard Membe alianza muhula wa pili wa Ubunge, Januari 2006, kama ‘front bencher’ baada ya kuteuliwa na rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani. Kufuatia mabadiliko ya baraza la Mawaziri mnamo mwezi Oktoba, 2006, Bernard Membe alihamishwa Wizara na kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini – moja ya wizara ngumu na nyeti kwa Taifa.
Hata hivyo miezi michache baadae, yaani January 2007, rais Jakaya Mrisho Kikwete alimteua Bernard Membe kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa baada ya aliyakuwa anashikilia wadhifa huo – Dr Asha Rose Migiro – kuteuliwa na Katibu Mkuu Baraza la Umoja wa Kimataifa na kuwa Naibu Katibu mkuu wa baraza hilo. Bernard Membe amehudu katika nafasi hiyo ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa tangu 2007 hadi 2015, akiwa ni Mtanzania wa pili kushika wadhifa huo kwa miaka mingi mfululizo, akitanguliwa na Rais Kikwete ambaye alidumu katika Wizara hiyo kwa miaka 10 mfululizo.