Yanga Mpeni Kocha Nabi Maua Yake




MPE maua yake, ndio msemo maarufu mtaani ukimaanisha mtu apewe sifa zake akiwa hai, na ndicho kinachotokea kwa kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi kwa kazi anayoifanya ya kutengeneza mastaa ndani ya kikosi hicho, baada ya kumfanya Clement Mzize kuwa miongoni mwa mastaa wanaofanya vizuri kwasasa ndani ya timu hiyo.

Si mara ya kwanza Yanga kupandisha vijana wa kikosi B huko nyuma walifanya baadhi yao ni Yusuph Mhilu aliyepo Kagera Sugar, Yusuf Athuman (Coastal Union, mkopo), Ramadhan Kabwili (Rayon Sports), Paul Godfrey 'Boxer' (SBS) hata hivyo hawakuanza kwa kasi kama ya Mzize.

Simba iliwahi kufurahia matunda ya kikosi B 2012 ilipandisha vijana wengi waliofanya vizuri, ingawa aliyesalia kikosini ni Jonas Mkude ambaye kapoteza namba, wengine wapo timu nyingine mfano Abdallah Seseme (Kagera) na wengine wengi.

Mzize hajachezea nafasi anayopewa na kocha wake na tayari katupia mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara akifunga dhidi ya Kagera Sugar, Polisi Tanzania, KMC, Geita Gold na Singida Big Stars.
Pia amefunga mabao sita kwenye Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), huku kocha wake akisema anamtengeneza kwa faida ya siku zijazo ndani ya kikosi chake na Taifa Stars.
"Namtengeneza kwa faida ya baadaye, kwa sasa anaendelea kupata uzoefu ambao utamsaidia kufanya mambo makubwa kwenye soka."
Makocha waliomnoa kikosi B, Fredy Mbuna na Said Maulid 'SMG' wanafurahishwa na maendeleo yake, wanayoamini yanawapa nguvu wengine kupambana zaidi.
Mbuna alisema; "Inatia moyo kuona kijana anaisaidia timu, inawapa moyo na wachezaji wengine kuzingatia kile tunachowafundisha wakiamini siku moja watafaidi matunda yao, ukizingatia kwa sasa soka ni ajira kubwa kwa wachezaji wote duniani."
Wakati SMG akisema pia; "Kikubwa azingatie anachoambiwa na kocha wake, kwani hiyo ni fursa kwake ya kufika mbali, binafsi nafurahia sana ninapomuona katoka kikosi B na anapata nafasi, inatupa moyo makocha kuendelea kupambana kuandaa wengine zaidi."
Yanga kama itatetea ubingwa msimu huu, ikifanikiwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika, ikifanikiwa pia kutinga fainali za Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), basi Mzize atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaobakia kwenye vitabu vya mashujaa wa Wanajangwani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad