YANGA imewasili alfajiri leo alfajiri ikitokea nchini Afrika Kusini walikoenda kufuzu fainali ya kwanza ya kihistoria ya klabu hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini kuna kauli ya jeuri wameitoa na kama wewe ni mtani wao basi utasonya kwa hasira, huku ikigoma kupangua ratiba ya mechi zao.
Yanga ina mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) itakayopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Liti, mjini Singida dhidi ya wenyeji Singida Big Stars na kulikuwa na tetesi huenda mechi hiyo ikasogezwa mbele kama ilivyo kwenye Ligi Kuu Bara, lakini mabosi wa Yanga kupitia benchi wamesema wanaenda kumalizana na Singida na fasta kuanza kujianda dhidi ya USM Alger.
Yanga kupitia kocha wao msaidizi Cedric Kaze ameliambia Mwanaspoti kuwa furaha ya kufuzu kwao kwenda fainali zimeishia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo jijini Johannesburg na kwamba malengo yao ni kombe la mashindano hayo yaliyopo mbele yao ikiwamo hiyo ya ASFC.
Kaze alisema hawataki kuweka kwenye akili zao kwamba wamepata mafanikio makubwa na kwamba baada ya ubingwa wa ligi wanayataka makombe yote ambayo wamebakiza likiwemo la Shirikisho na lile la Azam (ASFC) na hivyo kukomaa na ratiba zao kama zilizo ilio kufanikisha mambo.
"Hizi mechi mbili za nusu fainali tumezimaliza sasa akili yetu ni mechi zinazofuata, tulitaka kufuzu fainali lakini haya sio mafanikio kwetu, tutakuwa tumepata mafanikio kama tutachukua hili kombe, tunalitaka hili kombe tutaweka nguvu kubwa tulipate," alisema Kaze.
"Tunarudi kuendelea na mechi zingine na baada ya hapo tutaingia kwenye maandalizi ya mechi za fainali hizo mbili dhidi ya USM Alger, alisema Kaze huku bosi wake Nasreddine Nabi akakazia akisema wanatambua wanakwenda kukutana na timu bora lakini kikosi chake kimefikisha salamu kubwa kwa kushinda uwanja ambao wao waliushindwa.
USM Alger ikicheza mechi ya hatua ya makundi ugenini dhidi ya Marumo Gallants walipoteza kwa mabao 2-0 kabla ya Yanga juzi kuvunja mwiko huo wa Wasauz hao kutofungika kwao.
Yanga iliichapa Marumo kwa mabao 2-1 juzi na kuwafanya kuwang'oa kwa jumla ya mabao 4-1 kufuatia awali kushinda nyumbani kwa mabao 2-0.
Alger wao baada ya kuwalazimisha suluhu ASEC Mimosas ya Ivory Coast juzi wakashinda nyumbani kwa mabao 2-0 na sasa watakutana na Yanga katika mchezo wa kwanza wa fainali utakaopigwa Mei 28 Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya kurudiana wiki moja baadaye.
"Tunakwenda kukutana na timu ngumu USM Alger wana ubora mkubwa lakini Yanga haitakiwi kusemewa tena nayo imefanya makubwa ambayo kwasasa inazifanya kila timu kuiheshimu, tutazungumza zaidi juu ya mechi hizo mbili wakati ukifika lakini kwasasa akili zetu tunazipeleka kwenye mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida Big Stars," alisema Hersi.