Yanga Kuingia Fainali CAF Yasababisha Ligi Kuu Tanzania Kupanguliwa





KITENDO cha Yanga kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kimefanya ratiba ya Ligi Kuu Bara ipanguliwe kwa mechi za raundi mbili za mwisho kusogezwa mbele.

Yanga imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Marumo Gallants kwa mabao 2-1 ugenini na kuvuka kwa jumla ya mabao 4-1 baada ya awali kuifumua 2-0 jijini Dar es Salaam na sasa inajiandaa na mechi mbili za fainali dhidi ya USM Alger ya Algeria zitakazochezwa kati ya Mei 28 na Juni 3 mwaka huu.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Bodi ya Ligi (TPLB) kimeliambia Mwanaspoti kwamba kutokana na uwepo wa mechi hiyo muhimu na ya kihistiria kwa taifa, wameamua kusongeza mbele michezo yote ya raundi mbili zilizosalia zikihusisha timu zote.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali, mechi za raundi ya 29 na 30 zilipangwa kupigwa Mei 24 na 28 na Ligi ya msimu huu kumalizika, lakini kutokana na Yanga kukabiliwa kwa ratiba ngumu kwa wawakilishi wa mashindano hayo ya kimataifa wameamua kukaa chini na kusogezwa mbele kwa mechi zote.


"Mechi zilizobaki ili kukamilisha msimu huu zitapangiwa tarehe mpya baada ya kukamilika kwa mechi zote mbili za fainali kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye mashindano hayo ya kimataifa," kilisema chanzo hicho kilichokataa kutajwa jina gazetini na kuongeza;

"Hilo tayari limeshajadiliwa na kupitishwa ni ngumu kuruhusu ligi kuendelea ikiwa hii ni michezo ya kukamilisha msimu pamoja na bingwa kupatikana kuna timu zinapambana kubaki msimu ujao hivyo tunahofia upangwaji wa matokeo."

Chanzo hicho kiliongeza kuwa, kwa sasa TPLB, limefanya mchakato viziandikia barua timu zote zinazoshiriki ligi ili watambue mabadiliko hayo.

"Ligi zote duniani zimekuwa zikikamilisha michezo ya mwisho kwa kuchezwa pamoja haitaleta picha nzuri kukawa na viporo kwa kuruhusu michezo mingine iendelee kuchezwa alafu wapinzani wa Yanga waendelee kuwasubiri hadi hapo ratiba yao itakapokaa sawa;

"Mechi zilizobaki zitachezwa kwa wakati mmoja kama tulivyopanga ratiba ya kumaliza msimu hivyo mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa fainali wa Yanga na USM Alger tutatoa ratiba ya michezo hiyo ili kukamilisha msimu."

Yanga ambayo inakabiliana na Singida Big Stars katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la ASFC ilisaliwa na mechi mbili jijini Mbeya dhidi ya Mbeya City na Tanzania Prisons, huku Simba ikisaliwa na michezo miwili ya nyumbani dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad