Zitto akosoa wasifu wa Membe kutoitaja ACT-Wazalendo

 

Zitto akosoa wasifu wa Membe kutoitaja ACT-Wazalendo

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameonyesha kutoridhishwa na wasifu wa Bernard Kamillius Membe (69) kutogusia uwepo wake ndani ya chama hicho cha siasa.

Membe ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Kimataifa alijiunga na ACT-Wazalendo Julai 15, 2020 akitokea chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilichomlea. Hata hivyo, Mei 29, 2022 mwanasiasa huyo alirejea CCM.

Leo Jumapili, Mei 14, 2023, mwili wa Membe unaagwa Kitaifa katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kisiasa, wanadiplomasia na serikali wakiwemo, Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wake, Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Mara baada ya Zitto kuitwa kutoa salamu za rambirambi kwa niaba ya vyama vya siasa, alianza kwa kutoa angalizo kwamba atatumia zaidi ya muda uliopangwa wa dakika mbili.

“Sitaongea kwa dakika mbili, tunasherehekea maisha ya mtu aliyefanya mengi katika taifa hili. Sitaongea kwa niaba ya vyama vya siasa kwa sababu sijaongea nao kupewa hiyo ruhusa, nitaongea kwa niaba yangu binafsi kama mtu ninayemfahamu Membe na pia kama kiongozi wa chama ambacho Membe alikuwa mwanachama.

“Na ni muhimu sana historia iwekwe vizuri, maana nimemsikiliza jaji akisoma wasifu wa marehemu hajaweka kama Membe aliwahi kuwa mwananchama wa ACT -Wazalendo na alikuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita,” amesema Zitto.

Katika wasifu uliosomwa mbele ya waombolezaji eneo la siasa, umegusia kuwa amewahi kuwa mbunge wa Mtama kuanzia 2000 hadi 2015 na alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2020 na kuishia nafasi ya tano. Huku ukiacha ushiriki wake ndani ya ACT-Wazalendo pamoja na kugombea urais na ndicho kimemfanya Zitto kufafanua.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad