Algeria imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Uganda usiku huu Uwanja wa Omnisport Jijini Douala nchini Cameroon katika mchezo wa Kundi F kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Ivory Coast.
Mabao ya Algeria yote yamefungwa na mshambuliaji wa Lugano ya Uswisi, Mohamed El Amine Amoura dakika ya 42 na 66, wakati bao pekee la Uganda limefungwa na mshambuliaji wa Vyškov ya Jamhuri ya Czech, Fahad Aziz Bayo dakika ya 88.
Kwa ushindi huo, Algeria inafikisha pointi 15 na kuendelea kuongoza Kundi F kwa pointi nane zaidi ya Tanzania inayofuatia ikiwa na alama 7, wakati Uganda inabaki na pointi zake nne mbele ya NÃger yenye pointi mbili baada ya wote kucheza mechi tano.
Mechi za mwisho Septemba 4, 2023, Taifa Stars watakuwa wageni wa Algeria Jijini Algiers na Uganda watakuwa wageni wa Niger Uwanja wa Jénérali Seyni Kountché Jijini Niamey.
Stars inahitaji walau alama moja tu kukata Tiketi ya kucheza Michuano ya AFCON mwakani.