Uongozi wa Azam FC umekanusha taarifa za kuwa mbioni kumsajili Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kuachwa na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans.
Morrison alitajwa kuwa katika mipango ya Azam FC, saa chache baada ya kupewa Thank You na Uongozi wa Young Africans juma hili, lakini fasta Uongozi wa Azam FC umekanusha kuwa hauna mpango na kiungo huyo, ambaye pia aliwahi kuitumikia Simba SC.
Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo yenye maskani yake makuu Chamazi jijini Dar es salaam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ amesema Morrison hayumo kwenye orodha ya wachezaji wanaotakiwa na klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.
Popat amesema baada ya kumsajili kiungo mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei Toto’, wanatarajia kusajili wachezaji wa kigeni wawili au watatu kwenye nafasi ambazo zimeelekezwa na Benchi la Ufundi.
“Katika wachezaji wanaokuja Morrison hayumo.” amesema kwa kifupi Afisa Mtendaji Mkuu huyo. Hata hivyo ameainisha nafasi ambazo watazijaza kwa kufanya usajili katika kipindi hiki, ni beki wa kushoto, mshambuliaji mmoja na kiungo mshambuliaji mmoja.
“Msimu uliopita tulisajili wachezaji sita wa kigeni na wa ndani tisa kwa hiyo kikosi tunacho na kinajitosheleza, kilichopo ni kuongezea mapengo machache yaliyopo kama Benchi la Ufundi lilivyopendekeza na tutakuwa na maingizo ya wachezaji wa kigeni wawili, wakizidi sana watatu, kama ulivyoona beki wetu wa kushoto Bruce Kangwa ameondoka, hapo ni lazima tuingize mwingine na mbele pale tutasajili Mshambuliaji mmoja na kiungo mshambuliaji,” amesema Popat.
Katika hatua nyingine, Klabu hiyo imefanikiwa kuwaongezea mikataba Viungo James Akaminko, Sospeter Bajana na Beki wa pambeni Nathaniel Chilambo.
Chanzo: Dar24