Beki Avunja Mkataba Simba Apanda Ndege Kurejea nyumbani Kwao



BEKI mwili nyumba wa Simba, Mohammed Ouattara, ameona isiwe shida na kufikia makubaliano mazuri na klabu hiyo, ya kuvunja mkataba ili aondoke hapo Msimbazi.

Outtara ni kati ya wachezaji waliosajiliwa na Simba katika usajili mkubwa msimu huu akitokea Al Hilal ya nchini Sudan akisaini mkataba wa miaka miwili.

Beki huyo alisajiliwa na Simba kwa ajili ya kuiboresha safu ya ulinzi ya timu hiyo, lakini akashindwa na kufikia maamuzi hayo ya kuondoka.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani ya Benchi la Ufundi la Simba, Ouattara amekubali kuondoka Simba kwa makubaliano ya pande zote mbili kufikia muafaka.


Chanzo hicho kilisema uongozi wa Simba hivi sasa upo katika mazungumzo na baadhi ya mabeki wa kati watakaokuja kuchukua nafasi yake na kucheza pamoja na Mkongomani, Hennock Inonga.

Kiliongeza kuwa, sababu kubwa ya beki huyo kuondoka, ni kukosa nafasi ya kudumu ya kucheza katika kikosi cha kwanza, licha ya kuamini kiwango chake alichonacho yeye.

“Mazungumzo ya pande zote mbili baina ya beki Ouattara na Uongozi wa Simba yamefikia katika sehemu nzuri ya yeye kuondoka hapo baada yeye mwenyewe kuridhia.

“Siku yoyote kuanzia jana (Jumatano) alitarajiwa kupanda ndege kurejea nyumbani kwao huku akiweka mikakati ya kwenda kutafuta changamoto  sehemu nyingine.

“Ouattara hakuwa na msimu mzuri tangu ajiunge na Simba baada ya majeraha kumuandama mara kwa mara huku akipoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza,” kilisema chanzo hicho.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alizungumzia hilo kwa kusema: “Kila kitu kinachohusiana na usajili kwa hivi sasa kipo kwa kocha wetu Robertinho (Roberto Oliveira), na hivi karibuni kitawekwa wazi kila kitu baada ya taratibu kukamilika za kusajili na kuacha wale wachezaji wanaotakiwa kuachwa.”

STORI NA WILBERT MOLANDI

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad