Bunge la Tanzania Lahairishwa Kwa Muda Baada ya Kingora Cha Hatari Kulia Bungeni, Wabunge Wakimbilia nje

 




Bunge limeahirisha kwa muda kikaochake kilichokuwa kinaendelea leo Jumanne Juni 27, 2023 baada ya king'ora kinachoashiria kuna jambo la hatari kupiga kelele ndani ya ukumbi.


Ilikuwa ni saa 3.50 asubuhi wakati wabunge wakiendelea kwenye kipindi cha maswali na majibu ndipo king'ora kikalia na Spika, Dk Tulia Ackson akaahirisha shughuli za Bunge.


"Waheshimiwa wabunge hiyo sauti inaashiria tutoke humu ndani kwa haraka sana, kila mmoja atafute mlango wa kutoka na sote twendeni lile eneo la kukusanyikia, naahirisha shughuli za Bunge hadi hali itakapotulia," amesema Spika Dk Tulia.


Baada ya kurejea Bungeni, Spika amesema; "Waheshimiwa wabunge, nielezee jambo ambalo lilitufanya tukatoka nje na kuahirisha bunge kwa muda. Huu ukumbi wetu wa Bunge na majengo yote yamewekewa vifaa ambavyo vinaweza kutambua uwepo wa moshi au jambo lingine linaloweza kuleta athari hapa.


"Hapa tunapokaa wabunge kuna sehemu ya chini ambapo huwa kuna matumizi mbalimbali na kuna watu wanaotumia kule, kule chini kuna chumba kimoja wapo kilichokuwa na hitilafu ambapo wanafanya marekebisho, inabidi watindue hilo eneo.


"Katika kutindua vumbi likatoka, sasa vifaa vinavyonasa hitilafu vikanasa ile vumbi kama moshi ndio maana vikapiga kelele kuashiria kama kuna shida kwenye jengo hili.


"Nitumie fursa hii kuwajulisha kwamba jambo hilo limeshafanyiwa kazi, marekebisho yanaendelea lakini kwa utaratibu mzuri. Niwapongeze wabunge kila mtu ametoka nje kwa usalama na hakuna aliyeumia, na kila mmoja alielekea mlango ulio karibu yake na kutoka kwa utaratibu.


"Mbunge siku zote lazima ufahamu mlango ulio karibu na wewe, ukishatoka usibaki hapo inabidi uende sehemu salama zaidi ambazo zipo tatu kwa hapa Bungeni, ambapo ni kwa ajili ya kupata matangazo ya nini kimetokea na utaratibu utakuwaje," amesema Tulia.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad