Wakati deni la Serikali likipaa hadi kufikia Sh79.1 trilioni Aprili 2023 ikilinganishwa na Sh69.4 trilioni kipindi kama hicho mwaka jana, wachumi wameshauri umuhimu wa kushirikishwa sekta binafsi katika mikopo ili kupunguza athari zake.
Katika taarifa ya ‘Mpango wa Maendeleo 2023/2024’ iliyosomwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba inaonyesha ongezeko hilo la asilimia 13.9 linabebwa zaidi na deni la nje.
“Hadi kufikia Aprili 2023, deni la Serikali lilikuwa Sh79.1 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 13.9 ikilinganishwa na Sh69.4 trilioni kwa kipindi kama hicho mwaka jana,” alisema.
Dk Nchemba alisema kati ya kiasi hicho, deni la nje ni Sh51.1 trilioni na deni la ndani ni Sh27.9 trilioni na kwamba ongezeko hilo linasababishwa na mikopo ya miradi ya maendeleo kama vile barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme, elimu na afya.
Hata hivyo, katika bajeti pendekezwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga Sh6.31 trilioni kwa ajili ya kulipa deni lake, ambayo ni sawa na asilimia 14.21 ya bajeti pendekezwa ya Sh44.39 trilioni.
Kushuka uchumi
Wakati deni la Serikali likipaa, kasi ya ukuaji wa uchumi nchini imeshuka kwa asilimia 0.2 kutoka asilimia 4.9 mwaka 2021 hadi asilimia 4.7 mwaka 2022. Hata hivyo, makisio ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) yanaonyesha kuwa mwaka huu ukuaji wa uchumi wa Tanzania, utafikia asilimia 5.2, na hadi mwaka 2028 kasi itakuwa asilimia saba.
Kwa upande wa nchi nyingine za Afrika Mashariki, Kenya uchumi wake ulikuwa kwa asilimia 5.4 mwaka 2022 na Uganda ulikua kwa asilimia 4.9 katika kipindi hicho.
Hata hivyo, kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi hakujaiathiri Tanzania pekee, bali dunia kwa ujumla, taarifa ya IMF ya Aprili 2023 inaonyesha kasi hiyo kidunia imepungua kutoka asilimia 6.3 mwaka 2021 hadi asilimia 3.4 mwaka 2022.
Maoni ya wachambuzi
Akizungumzia ongezeko la deni la Serikali na kudorora kwa ukuaji wa uchumi, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Aurelia Kamuzora alisema kupaa kwa deni siyo jambo la kushangaza, kwa sababu linafanya miradi ya maendeleo.
“Kwa nchi kukopesheka ni baraka, lakini ukikopa na kutumia vibaya basi kunaharibu uchumi, sisi tumekopa na tunawekeza hadi uchumi umeendelea kukua kwa zaidi ya asilimia nne. Ukuaji huu unategemea fedha zilizoingizwa kwenye miradi ya maendeleo,” alisema.
Profesa Kamuzora alisema nchi ikikopa lazima deni liwe kubwa na manufaa hayawezi kuonekana kwa haraka. Deni linaweza kujilipa baada ya miaka 10 au 20, akitolea mfano wa mradi wa bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere ambalo amesema mchango wake hautaonekana hivi karibuni.
Alisema kwa kuwa ukuaji wa uchumi bado ni chanya, deni la Serikali litaanza kujilipa baada ya muda.
Mawazo yake yaliungwa mkono na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dk Lawi Yohana aliyesema ongezeko hilo linasababishwa na miradi mikubwa inayotekelezwa sasa na Serikali, ikiwamo ujenzi wa reli ya kisasa ambao mapato ya kodi ya ndani hayawezi kugharimia miradi hiyo.
“Ukiangalia ni kiasi gani tunaweza kukusanya sisi wenyewe na ukaangalia matumizi ya kawaida ya kulipa deni la nje ni kidogo, hivyo Serikali inalazimika kutafuta fedha nje kuja kugharimia miradi hiyo,” alisema.
Sekta binafsi yatajwa
Naye mchambuzi wa masuala ya uchumi, Oscar Mkude akizungumzia ongezeko la deni la Serikali, alisema si lazima Serikali iendelee kukopa peke yake, bali izishirikishe sekta binafsi katika miradi ya maendeleo.
“Kwa miradi ambayo inatekelezwa kwa fedha za mikopo ni muhimu Serikali isimamie miradi hiyo ili ianze uzalishaji kwa wakati,” alisema.
Mkude alisema kwa kipindi kirefu Tanzania imekuwa ikipata hasara kutokana na matumizi ya ndani kuwa makubwa kuliko makusanyo na kutoa fedha nyingi nje kuliko inayoingiza.
“Sasa ili kutekeleza miradi ya maendeleo Serikali inakopa kwa sababu haina fedha za ndani za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo, jambo la kufanya ni kuangalia miradi ya maendeleo kwa namna ambayo imepangwa ili ianze kuleta tija,’’ alisema.
Mkude alisema ili miradi inayotekelezwa kuanza kuonyesha tija ni ujenzi wake kuzingatia njia sahihi ya watu kutumia miundombinu kusafirisha mizigo na kulipa kodi.
Kwa upande wake, Dk Yohana alishauri mikopo inayochukuliwa ilenge kuchochea miradi ya kimkakati ambayo itagusa sekta nyingine ili iweze kulipunguza deni hilo.
Mbali na mjadala wa kupaa kwa deni la Serikali na kushuka kwa ukuaji wa uchumi, Dk Mwigulu akiwasilisha bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/24 bungeni juzi, alisema bado deni ni himilivu.
“Tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika Desemba, 2022 imeonyesha kuwa deni ni himilivu na viashiria vya deni viko ndani ya wigo unaokubalika kimataifa katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu,” alisema.
Aprili, mwaka huu, Mkurugenzi Msaidizi wa IMF, Antoinette Sayeh wakati akiidhinisha mkopo wa dola 153 milioni (Sh358.9 bilioni) kusaidia utekelezaji wa bajeti ya Serikali nchini, alisema deni la Tanzania bado ni himilivu na la wastani.
“Deni la Tanzania bado ni la wastani na himilivu, lakini ni muhimu kuendelea kuweka kipaumbele katika mikopo yenye riba nafuu,” alisema.