KUELEKEA mchezo wa fainal ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya USM Alger utakaopigwa leo Jumamosi nchini Algeria, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said ametamba kuwa licha ya kipigo cha mabao 2-1 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wana matumaini makubwa ya kupindua meza kama walivyofanya dhidi ya Club Africain ya Tunisia.
Yanga ambao waliondoka nchini juzi Alhamisi ambapo leo Jumamosi wanatarajia kushuka kwenye Uwanja wa 5 July 1962 kuvaana na USM Alger, katika mchezo wa fainali ya mkondo wa pili unaotarajiwa kupigwa majira ya saa 4 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Kikosi hicho kinaingia katika mchezo wa leo wakiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa fainali ya kwanza kwa kipigo cha mabao 2-1, mchezo uliopigwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Hersi alisema: “Tupo tayari kwa ajili ya mchezo huu muhimu, kama timu tunajua wapi tulipoteleza kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza na tayari tumefanya marekebisho na tunaamini huu utakuwa mchezo tofauti.
“Kuna baadhi ya watu wanadhani mchezo umeisha kwa kuwa tulipoteza mabao 2-1 nyumbani, lakini niwahakikishie kuwa tuna nafasi ya kuwashangaza watu kwa kupindua meza hapa Algeria kama ambavyo tulifanya dhidi ya Club Africain kule Tunisia.”
Stori na Joel Thomas