Fiston Mayele awajibu waliombeza 2022/23

Fiston Mayele awajibu waliombeza 2022/23


Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele ameibuka na kutamka kuwa tuzo tano alizoshinda msimu uliopita wa 2022/23 zimethibitisha ubora wake, huku akiwashukuru viongozi, wachezaji na mashabiki wa Young Africans.

Mshambuliaji huyo alirejea nchini juzi Jumanne (Juni 20) saa sita mchana akitokea DR Congo alipokwenda katika majukumu ya timu ya taifa hilo, iliyocheza dhidi ya Gabon katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’.

Tuzo hizo alizoshinda mshambuliaji huyo ni Mchezaji Bora, Mfungaji Bora, Bao Bora, Kikosi Bora cha msimu na Ufungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Mayele amesema waliokuwa wanabeza ubora wake, umethibitishwa na tuzo hizo alizozibeba katika msimu uliopita ambao kwake ulikuwa na mafanikio makubwa.

Mayele amesema kuwa ubora wake haujatosha pekee, shukrani nyingi amezitoa kwa wachezaji wenzake waliompa ushirikiano wa kutosha uwanjani ikiwemo pasi nzuri za kufunga.

Ameongeza kuwa hajaridhirika na mafanikio mazuri aliyoyapata msimu huu, bado ana mengi ya kuyafanya katika msimu ujao kama akibakia kuendelea kuichezea timu hiyo.

“Tuzo ambazo nimeshinda katika msimu uliopita, zimethibitisha ubora wangu, na hilo lipo wazi kila mtu aliona jinsi nilivyoipambania timu yangu ya Young Africans na kufanikiwa kushinda Tuzo.

“Niwashukuru viongozi, wachezaji wenzangu, mashabiki pamoja na benchi la ufundi ambalo lilihakikisha ninakuwa bora wakati wote kwa kuniandaa vema kabla ya mchezo.

“Bado sijafanikiwa na haya mafanikio ambayo nimeyapata, bado nina kibarua kigumu cha kupambana ili nipite zaidi ya mafanikio haya,” amesema Mayele.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad