Hapa tu Ndio Yanga Walipoishindia SIMBA Msimu Uliopita Nje na Ndani ya Uwanja

Hapa tu Ndio Yanga Walipoishindia SIMBA Msimu Uliopita Nje na Ndani ya Uwanja


Yanga imeendeleza ubabe wake ndani ya msimu huu wakichukua taji la pili la ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutoka kwa watani wao Simba ambao mapema wekundu hao walichukua taji hilo mara nne mfululizo.

Watani wao Yanga wanaendelea kukimbiza rekodi hiyo baada ya msimu huu tena kulirudisha taji hilo ndani kwao, lakini safari hiyo ya Yanga kufanya vizuri kumetokana na sababu nyingi za mabadiliko chanya ndani ya kikosi hicho cha wananchi.

USAJILI

Yanga ilianza kwa kuwazidi Simba kupitia eneo la usajili, kwa mwaka wa pili sasa Yanga imeendeleza ubora wa kikosi chao huku wekundu hao wakiendelea kuanguka taratibu kwa kukosa hesabu sahihi za kusuka kikosi chao.

Ubora wa kikosi cha Yanga halikuwa suala la usiku mmoja bali walikuwa na muendelezo wa hesabu sahihi za maboresho ya kikosi chao, ukiangalia ubora wa Yanga ilinzia msimu wa juzi ambao walimaliza wa pili wakati Simba ikichukua ubingwa wa mwisho.

Msimu uliofuata Yanga waliendelea kuleta mastaa wakubwa zaidi ambao wakawapa ubingwa wa kwanza kutoka Simba lakini hawakuishia hapo msimu huu wakaendeleza maboresho zaidi ambayo yakakiongezea thamani kikosi chao.

Ujio wa mastaa kama Kennedy Musonda, Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sureboy’ Stephanie Aziz KI, Joyce Lomalisa, walikuja na kitu kikubwa zaidi kuwapa ubora Yanga huku Simba wao wakiangushwa na mastaa wengi ambao walishindwa kuwa na kasi kubwa ya kuongeza ubora wa kikosi chao kiushindani.

Simba ilitegemea makubwa kuipindua Yanga kupitia usajili wa Habib Kyombo, Nelsomn Okwa, Augustine Okrah, Victor Akpan, Ismael Sawadogo, Mohamed Outtara walishindwa kuwa na kasi kubwa ya kuipuigania klabu hiyo na baadhi kuondolewa huku wengine wakisotea benchi.

BENCHI LA UFUNDI IMARA

Eneo lingine kubwa lililowabeba Yanga ni utulivu na ubora wa benchi lao la ufundi chini ya kocha Nasreddine Nabi, akisaidiwa na Cedric Kaze, Milton Nienov, Helmy Gueldich kisha baadaye wakamuongeza mtaalam mwingine Khalil Ben Yousef ambao utaanzia kuwaheshimu kwa kudumu kwao kwa muda mrefu lakini pia ubora wao kutengeneza kikosi imara.

Simba mambo yalikuwa tofauti kwanza kulikuwa na muendelezo wa ujio wa makocha na kuondoka kwa haraka katika kipindi kifupi ambacho kiliipotezea timu utulivu kwa kuwa kila kocha alikuwa na falsafa zake hatua ambayo ilichangia pia hata kuwapoteza wachezaji kuweza kusomeka.

UPANA WA KIKOSI

Hili pia lilijidhihirisha Yanga lakini pia ilijionyesha kuwa changamoto katika kikosi cha Simba, Yanga walikuwa na kikosi kipana ambacho kiliwabeba lakini kubwa zaidi makocha wao walipambana kuondoa utofauti wa ubora kutoka mchezaji mmoja kwenda mwingine.

Kila timu ilipitia kipindi kigumu cha kuwa na majeruhi lakini Yanga haikuonekana kuathirika sana kutokana na makocha wao kuondoa tofauti kati ya mchezaji aliyekuwa anaanza na atakayeingia, wapo ambao ubora wao ulizidi kuwa chini ambao baadaye hawakuonekana kabisa.

Simba hali haikuwa hivyo kama kwa watani wao alipokosekana mchezaji ambaye alikuwa anacheza kwa muda mrefu kuna wakati timu ilionekana kukosa mtu bora wa kuziba nafasi yake kwa ufanisi kama wa yule wa awali ambaye ametoka hii iliipunguzia Simba kasi yake.

VIWANGO BORA VYA WACHEZAJI

Wachezaji nao wewnyewe viwango vyao ni kitu ambacho kiliwanufaisha Yanga ukiwaangalia mastaa wao walikuwa katika viwango vikubwa na muendelezo ulio bora kitu ambacho kwa upande mwingine kiliwaathiri Simba.

Sio kwamba Simba mastaa wao hawakuwa bora lakini walikosa kuwa na muendelezo mzuri wa viwango vyao mfano mzuri akiwa Okrah ambaye alianza kwa kasi nzuri lakini baadaye akapotea, hivyo hivyopia ilimtokea Mosses Phiri baada ya kuumia na hata aliporudi alishindwa kurudisha kiwango chake.

MPASUKO SIMBA

Ukiitazama Yanga ilikuwa na utulivu mkubwa katika uongozi wake kuanzia Rais wao injinia Hersi Said, kamati yake ya utendaji hali hiyo ikaleta utulivu mkubwa kwenye sekretarieti yao chini ya Mzambia Andre Mtine ambaye ni Afisa Mtendaji wao mkuu.

Tangu ujio wa Mtine msimu huu akichukua kijiti cha Msauz Senzo Mazingiza ambaye alitimka mwisho wa msimu uliopita, Yanga iliendeleza utulivu wake kwa kila idara kufanya kazi zake kwa nafasi hatua ambayo iliwanufaisha tena msimu huu.

Hili ni tofauti na Simba ambao baada ya kuanza kwa utulivu msimu walijikuta baadaye wanakumbana na changamoto za kiungozi kwa migogoro ya ndani kwa ndanmi kuwatafuna wakionekana kupingana, anzia pale mpaka alipoondoka aliyekuwa Afisa mtendaji wao mkuu Barbara Gonzalez ambaye kabla ya kutimika kulitangulia vuguvugu zito.

Hata baada ya Barbara kuondoka ukaja uchaguzi mkuu wa uongozi wa juu wa uoande wa wanachama ambao nao ukaliongeza tatizo kwa kuibuka mpasuko mkubwa kwa baadhi ya vigogo wazito kupingana na kuzalisha makundi ndani ya klabu yao, hili liliathiri timu yao na kujikuta kuna wakati muda unatumika kuwekana sawa na sio tena kutafuta maendeleo.

NIDHAMU YA WACHEZAJI

Yanga ukiondoka sakata la kujiondoa kwa kiungo wao mshambuliaji Feisal Salum ‘Fei toto’ hakukuwa na shida kubwa ya nidhamu na hata ilipojitokeza kidogo ilikuwa rahisi kutuliza hali hiyo ndani kwa ndani lakini kule Simba mambo yalikuwa tofauti kidogo wapo wachezaji walisumbua kwa nidhamu hatua ambayo iliipunguzia kasi.

Inasemekana hata huku mwishoni mwa msimu kuliibuka hali ya baadhi ya wachezaji kujitengenezea mazingira ya kutaka kuwahi kwenda makwao wakitafuta kadi za makusudi lakini pia Okraha ambaye amekuwa mchezaji wa kwanza kusitishiwa mkataba alitajwa kuwa na shida ya nidhamu ndani ya kikosi hicho.

HESABU ZA YANGA UGENINI

Yanga ukiacha kushinda mechi nyingi nyumbani na ugenini lakini waliwaacha Simba katika mechi za ugenini zaidi wakishinda mechi 11 kabla ya mechi mbili za mwisho wakati watano wao wakishinda mechi 9 pekee.

Simba iliangushwa sana na sare zao walizopata ugenini wakitoa jumla ya sare 5 na kupoteza mechi moja ambazo ziliwasababishia kuangusha alama 13 wakati Yanga wao ugenini waliangusha alama 6 pekee baada ya kupoteza mechi mbili.

Nyumbani nako Yanga iliangusha alama nne pekee baada ya kutoa sare mechi mbili huku mechi zingine zote 13 wakati Simba wao nyumbani walishinda mechi 12 wakipoteza alama mbili pekee baada ya kutoa sare mechi moja.

MZUKA WA CAF

Inaweza kuwa imewachangia Yanga kuwa bora zaidi kwenye ligi kwa kuwa katika mashidano ya Afrika husan Kombe la Shirikisho walikuwa na kiwango bora kushinda miaka yote tangu klabu hiyo ianzishwe, msimu huu ambao walicheza fainali na kushika nafasi ya pili walipoteza mechi mbili pekee ambapo moja ilikuwa hatua ya makundi dhidi ya US Monastir lakini mchezo mwingine ni wa fainali ya kwanza hapa nyumbani.

Yanga walipokuwa wanashinda kwenye mechi za CAF walikuwa wanarudi na mzuka kwenye ligi na kuendeleza matokeo yao mazuri lakini Simba wao ikawa tofauti hasa baada ya kuishia tena hatua ya robo fainali iliwapunguzia morali ya kuendelea kupambana huku wakijikuta wana mlima mkubwa baada ya watani wao kuwaacha kwa alama nyingi kwenye mbio za ubingwa wa ndani.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad