Mastaa wanaokipiga Ligi Kuu Bara wamewakilisha vyema timu zao za Taifa katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zitakayofanyika mwakani nchini Ivory Coast.
Ligi Kuu Bara imetoa wachezaji wengi ambao wameitwa timu zao za Taifa na wamefanikiwa kufuzu Afcon, Simba ni Clatous Chama, Henoc Inonga na Pape Sakho na Yanga ni Fiston Mayele, Djigui Diarra, Kennedy Musonda, Khalid Aucho na Azizi KI.
Senegal inayoongoza kundi L na pointi 13 inawakilishwa na mastaa kama Sadio Mane anayekipiga Bayern Munich, Kalidou Koulibaly na kiungo mshambuliaji wa Simba Pape Sakho ni moja ya timu zilizofuzu mapema kucheza Afcon 2023.
Zambia 'Chipolopolo' ilifuzu juzi ikiwa nyumbani kwa kuichapa Ivory Coast mabao 3-0 uwanja wa Levy Mwanawasa, ikiongoza kundi H na pointi 12.
Kikosi hicho cha Chipolopolo kinawakilishwa na mastaa Clatous Chama ambaye ni kiungo tegemezi Simba huku Yanga ikiwakilishwa na mshambuliaji wake Kennedy Musonda.
Timu ya taifa ya Mali inawakilishwa na mlinda mlango wa Yanga, Djigui Diarra amefanikisha Mali kufuzu Afcon baada ya kumaliza mchezo bila kuruhusu bao na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 uwanja wa Stade Alphonse Massemba-Débat nchini Congo
Timu ya taifa ya kiungo wa Yanga Azizi KI, Burkina Faso imefuzu Afcon mapema licha ya mchezo wa jana kutopata matokeo dhidi ya Cape Verde na kufungwa mabao 3-1 lakini inaongoza kundi B ikiwa na pointi 10 huku ikipoteza mechi moja na sare moja
Licha ya mastaa hao kujihakikishia tiketi hiyo, wapo wengine ambao timu zao bado hazijafuzu Afcon ambazo ni Taifa Stars (Tanzania), DR Congo inayowakilishwa na beki wa Simba Henoc Inonga na mfungaji bora Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu, Fiston Mayele wa Yanga ambaye jana ameipa timu yake bao dakika ya 83 akitokea benchi.
Uganda pia inayowakilishwa na Khalid Aucho bado ina mechi ya mkononi itakayoamua kati yao na Taifa Stars nani ataenda Ivory Coast.