Rais wa Young Africans Injinia Hersi Saidi, amesema wanatambua baadhi ya wachezaji wao muhimu akiwamo mshambuliaji Fiston Mayele wako katika siku za mwisho za mikataba yao na tayari wameshaanza mazungumzo kwa ajili ya kuhakikisha wanawabakiza klabuni hapo.
Hersi amesema watatumia njia tatu’ ili kuhakikisha wanamshawishi mchezaji huyo kubakia Jangwani kwa kumwandalia mazingira mazuri katika mkataba wake au wanamuuza na kutafuta mtu sahihi’ atakayechukua nafasi yake.
“Tunajivunia mchezaji wetu kutakiwa na timu zote kubwa za Afrika, ingeshangaza tufanye vizuri halafu isiwe kocha wala mchezaji wetu kutakiwa na timu nyingine, kama ikitokea hilo tunahakikisha tunazungumza na mchezaji ili kumbakiza ndani ya kikosi kulingana na mahitaji ya benchi la ufundi,” amesema Hersi.
Rais huyo ameongeza wachezaji wa Young Africans kutakiwa na timu nyingine ni sehemu ya mafanikio kwa sababu inadhihirisha wana kikosi imara.
“Viongozi tuko makini katika kuhakikisha tunawabakiza baadhi ya wachezaji wetu ambao mikataba yao iko ukingoni, usajili wetu huu tutachukua nyota wenye kiwango bora ambaye atakuja kuongeza kitu kwenye kikosi,” Hersi ameongeza.
Kuhusu mipango msimu ujao ujao katika mashindano ya kimataifa, amesema kiongozi huyo ya malengo yao ni kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.