Baada ya miaka 13 Jonas Mkude anaondoka Simba. Mambo hufika mwisho na Mkude ataonekana akiwa na jezi tofauti na ile Simba. Nani aliwahi kufikiria kwamba yule mtoto pendwa wa Msimbazi siku moja ataondoka na mashabiki hawataumizwa na kuondoka kwake?
Miaka mitano iliyopita, Mkude alikuwa lulu Simba na kila mtu Simba alimpenda. Leo Mkude anaondoka Simba mashabiki waliompenda miaka mitano iliyopita wenyewe wakiwa hawamtaki.
Angeondoka miaka mitano nyuma mashabiki wangeungana kuumeza uongozi wa Simba. Hapa tunapata suala la kwanza la kujadili. Maisha ya mwanasoka ni mafupi na unapendwa kipindi upo katika ubora wako.
Siyo tu Tanzania, bali dunia nzima. Hapa tunajifunza kwamba mwanasoka anapokuwa katika ubora akazane kuvuna pesa za kutosha kwa sababu watu wa mpira hawana shukrani.
Unapofika mwisho hawakutaki na hawakumbuki mazuri uliyofanya kipindi wanakupenda. Unapaswa kuwa katili unapokwenda katika meza ya mazungumzo. Hata kina Steven Gerrard walikuwa mashabiki wa Liverpool, lakini walikuwa jeuri lilipokuja suala la maslahi yao.
Kuna hili lingine. Mkude alianza kucheza Simba ya watoto kabla ya kupandishwa katika timu ya wakubwa. Ni kipindi kile Simba ikipambana na bajeti finyu walipoamua kutumia vijana. Wachache wakafanikiwa mmoja akiwa Mkude.
Mkude ameweza vipi kudumu Simba kwa miaka 13? Ni ngumu sana kudumu Simba na Yanga kwa miaka mingi, lakini Mkude ameweza. Hesabu wachezaji waliodumu sana wangapi wamefikisha miaka 13?
Ni lini Simba wamezalisha mchezaji imara kutoka timu ya vijana kama ilivyokuwa kwa Mkude? Suala la pili la kujiuliza. Wengi wanaozalishwa kutoka timu za vijana huwa hawadumu au kupata nafasi za uhakika katika klabu zao.
Unaweza ukawatazama waliopandishwa Simba ya wakubwa pamoja na Mkude. Wangapi wamefika alipofika Mkude? Kuanzia kwa Ibrahim Ajib, Said Ndemla, Haruna Chanongo na Ramadhan Singano wangapi wamedumu kama Mkude?
Ndiyo! Kina Ibrahim Ajib wamejitahidi lakini ni lini walikuwa sehemu muhimu ya timu kama alivyowahi kuwa Mkude. Miaka ya karibuni ambayo Simba wamefanya vyema katika mashindano ya kimataifa Mkude alikuwa mmoja kati ya wazawa wachache waliounda safu imara ya kiungo ya Simba.
Kama Simba wasingekuwa na Mkude wangelazimika kwenda nje ya nchi kutafuta kiungo wa kucheza eneo lake. Huyu ni mchezaji aliyetengenezwa na Simba. Kumbe kuna nyakati unaweza ukaokoa pesa nyingi za usajili kwa kutengeneza wachezaji wako wenyewe.
Hapo katika wachezaji wa kigeni linaibuka suala lingine. Mkude aliweza vipi kushindana na wageni katika eneo la kiungo la Simba? Licha ya ubora mkubwa wa Mkude bado kuna kipindi Simba walisafiri kuleta viungo wa kushindana naye.
Hawa ndio kina Tadeo Lwanga, James Kotei na Gerson Fraga. Bado katika uwepo wa wageni Mkude alichomoza na kuchukua nafasi katika kikosi. Leo hii tuna wachezaji wengi wazawa wanaofurahia kukaa katika mabenchi ya timu kubwa huku nafasi zao zikitawalia na wageni. Mkude hakukubali hiki kitu.
Wapo wachezaji wachache waliofanikiwa kushindana na wageni katika klabu kubwa. Shomary Kibwana, Hassan Dilunga, John Bocco na Feisal Salum 'Feitoto' ni kati ya wazawa wachache waliofanikiwa kufurukuta na kuchomoza mbele ya wageni.
Kitu cha mwisho cha kukitazama kwa Mkude ni jinsi ambavyo alikosa nafasi ya kuwa nahodha wa Simba kipindi ambacho pengine alipaswa kuvaa kitambaa cha unahodha. Mkude ni kiongozi halisi na kuna kipindi alikuwa nahodha wa Simba, lakini kwa sababu zinazodaiwa kuwa za kinidhamu alipokonywa kitambaa. Hapo akakosa hadi nafasi ya kuwa nahodha msaidizi.
Hata alipokuja John Bocco tayari Mkude alikuwa na miaka saba klabuni. Alikuwa nahodha na alipaswa kuendelea kuvaa kitambaa, lakini haikuwa hivyo. Hata nahodha mkuu wa Simba alipokosekana bado kitambaa kilienda kwa Mohammed Tshabalala na si Mkude.
Mchezaji mwandamizi anayeifahamu vyema klabu na mwenye mamlaka katika chumba cha kubadilishia nguo hupewa kitambaa cha unahodha, lakini haikuwa hivyo kwa Mkude. Ni kama ambavyo imetokea kwa Granit Xhaka pale Arsenal. Unafikiri kituo kipi kinafaa kwa Mkude?