Kakolanya Aliyekuwa Kipa wa Simba Afuguka "Nilituhumiwa kuuza mechi"

 

Kakolanya Aliyekuwa Kipa wa Simba Afuguka "Nilituhumiwa kuuza mechi"


Aliyekuwa kipa wa Simba, Beno Kakolanya ameweka wazi katika maisha yake ya soka aliwahi kutuhumiwa kuuza mechi japo jambo hilo si la kweli.

Kakolanya amefanya mazungumzo hayo baada ya kuwa mchezaji huru kutokana na kumaliza mkataba wa kuitumikia timu hiyo mwezi huu.

Akizungumza Dar es Salaam, Kakolanya alisema kutumiwa kuuza mechi kulianza tangu akiwa na kikosi cha Tanzania Prisons na hata alivyokwenda Yanga.

"Nikiwa Prisons kocha wetu akiwa marehemu Mwamwaja (David) aliwahi kuniambia mimi na meneja wangu tumeuza mechi dhidi ya Simba, lakini ilimalizika kwa suluhu ya bila kufungana.

"Hata nikiwa na Yanga pale kocha wetu Zahera (Mwinyi) aliwahi kunifuata na kuniambia hanichezeshi kikosi cha kwanza kwa sababu ameambiwa meneja wangu ni Simba, mimi nilimuambia mbona mechi ambayo ilikuwa ngumu halafu Yanga haikuwa nzuri na Simba ilikuwa bora hatukufungwa ndipo Zahera alinielewa," alisema Beno.

Akizungumzia hatma yake ndani ya Simba, kipa huyo wa zamani wa Yanga alisema tayari ameshamaliza mkataba na timu hiyo, huku hatma ya msimu ujao ikifahamika baada ya usajili kufunguliwa.

"Ningekuwa na mkataba Simba nisingeweza kuongea kwa sababu kuna vipengele ambavyo vinatubana, nimeshamalizana nao na kuhusu msimu ujao basi tusubiri.

"Najivunia kucheza Simba kwa sababu nimejifunza vitu vingi hasa kimataifa, nimecheza mechi chache, lakini hata kuwa benchi nimeona wenzangu nini wanachofanya, mimi naweza kuwa bora kwenye kitu fulani na mwengine akawa na ubora tofauti na niliona," aliongeza.

Kwenye mechi za mwisho baada ya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula kuumia, wengi walitarajia kumuona langoni, lakini nafasi yake akawa Ally Salim (kipa namba tatu), huku akidaiwa sababu kubwa ni kusaini mkataba na Singida Fountain Gate.

Akizungumzia jambo hilo alisema kwa upande wake ana amini kabisa Ally alikuwa kwenye wakati mzuri licha ya kwamba kuna baadhi ya mechi alifanya makosa madogo madogo.

Kakolanya amedumu katika kikosi cha Simba kwa misimu minne mfululizo baada ya kuwa mchezaji huru akitokea klabu ya Yanga 2019.

Kipa huyu inadaiwa ameshamalizana na mabosi wa Singida Fountain Gate kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu kwa mkataba wa miaka miwili.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad