Huku wakiwa kwenye mchakato wa kupitia wasifu (CV) za makocha ambao wametuma maombi ya kuifundisha Yanga, uongozi wa timu hiyo umeibuka na kuweka wazi kuwa kocha mkuu mpya atakayekuja ameandaliwa malengo makubwa mawili ambayo atapaswa kukubaliana nayo kabla ya kusaini mkataba.
Uongozi wa Yanga kwa sasa umeingia chimbo kusaka kocha mpya ambaye anakuja kuchukua nafasi ya aliyekuwa kocha wao mkuu, Nasreddine Nabi ambaye ameondoka ndani ya timu hiyo mara baada ya kumalizika kwa mkataba wake.
Yanga usiku wa kuamkia juzi Alhamisi walitangaza kufikia makubaliano ya kuachana na kocha Nabi ambaye ameiongoza Yanga kwa kipindi cha msimu miwili na nusu huku akifanikiwa kukusanya mataji sita na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza nasi, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema: “Kwanza tunaendelea kumtakia kila la kheri aliyekuwa kocha wetu mkuu Nasreddine Nabi na kumshukuru kwa kipindi chote alichokuwa nasi.
“Kwa sasa hayo yameisha na nguvu kubwa ya uongozi ni katika kuhakikisha tunamtafuta mbadala wake ambaye atapewa mitihani mikubwa miwili.
“Kwanza kuhakikisha timu inaendeleza utawala wake kwenye mashindano ya ndani (ambapo washindani wao wakubwa ni Simba) na wa pili ni kuhakikisha timu inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao jambo ambalo tumeshindwa kulifanya kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita.”