Unaambiwa baada ya uongozi wa Yanga kumpa taarifa kocha mkuu mpya wa timu hiyo raia wa Argentina, Miguel Angel Gamondi, ambayo ilitakuwa kuwa Julai 17, mwaka huu, mwenyewe amegoma akisema hadi akitua nchini ndipo atajua kambi inaanza lini.
Yanga kabla ya kuachana na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi, ilipanga kambi ya maandalizi ya msimu ujao itakuwa nchini Tunisia kuanzia Julai 17, mwaka huu, lakini baada ya Nabi kuondoka na Gamondi kurithi mikoba yake, ratiba imebadilika.
Chanzo kutoka Yanga, kimetonya kwamba: “Tayari kocha kashaanza kutekeleza majukumu yake ambapo amezuia kambi kuanza Julai 17 na kuwataka viongozi wamsubiri hadi atakapotua nchini wiki hii.
“Kocha amesema atakapotua, ndipo atapanga mwenyewe namna kambi itakavyokuwa na apate muda wa kuzungumza zaidi na viongozi watu atakaoambatana nao kambini.”
Ikumbukwe kuwa, Jumamosi ya wiki iliyopita, Yanga ilimtangaza kocha huyo kurithi mikoba ya Nabi ambapo sasa ana jukumu la kutetea mataji yote waliyobeba Yanga msimu wa 2022/23 ambayo ni Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
Pia jukumu lingine ni kuhakikisha Yanga inacheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023/24, kama yalivyo malengo ya uongozi.