Nchini Norway katika mji wa Halden lipo gereza maarufu la Halden linalotajwa kuwa gereza lenye utu zaidi duniani.
Gereza hilo lililojengwa kwa lengo la kurekebisha tabia za wafungwa na kukuza uwezo wao, ni mahali penye ulinzi mkali panapojulikana kwa mbinu yake ya kibunifu na ubinadamu kwa wafungwa.
Muundo wa Gereza la Halden unafanana na kijiji kidogo badala ya gereza kama ilivyozoeleka.
Wafungwa katika gereza hilo wanaishi katika mazingira ya kisasa huku kila mmoja akiwa na chumba chake chenye choo na bafu, madirisha makubwa kwa ajili ya hewa pamoja na maeneo ya jumuiya kama jiko la kisasa na viwanja vya mazoezi vya kuwakutanisha wafungwa wote.
Gereza hilo linasisitiza wafungwa kuisha kama raia wa kawaida na kufanya shughuli zao za kila siku ikiwa ni pamoja na kupika na kufanya usafi, , na kupata fursa za burudani kama vile michezo, muziki na kuangalia bustani.
Zaidi ya hayo, wafungwa wana fursa za kujifunza ujuzi mpya na kupata mafunzo ya ufundi stadi ili kupata mwanga wa wapi pa kuanzia watakapotoka gerezani.