Lissu: Ni mkataba wa hovyo kuwahi kutokea




Dar es Salaam. Makamu Mwenyeki wa Chadema, Tanzania Bara, Tundu Lissu amekosoa makubaliano kati ya Serikali za Tanzania na Dubai kwa ajili ya uboreshaji na uendeshaji wa bandari yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, akisema ni ya hovyo katika historia ya Tanzania.

Lissu ameeleza hayo leo Juni 10, 2023 wakati akizungumza na Mwananchi kupitia mtandao wa WhatsApp, akisema ni mkataba usioweza kuvunjwa au kusitishwa hata kama nchi hii ikivunja uhuasiano wa Kibalozi/Kidiplomasia na Dubai/UAE na hata kama nchi ikiwa vitani au katika mazingira mengine yoyote.

"Huu ni mkataba wa hovyo kuliko mikataba mingine yote iliyopata kusainiwa na Serikali ya Tanzania katika historia yetu yote tangu uhuru.” Amesema na kuongeza;

"Ni mkataba unaobadilisha Katiba na Sheria za nchi yetu kuhusu masuala ya bandari. Ni mkataba unaojiweka juu ya sheria na mikataba ya kimataifa ambayo nchi yetu ni mwanachama wake," amesema Lissu.


Lissu ambaye alikuwa Mgombe Urais wa Chadema mwa 2020, amebainisha kwamba kimsingi huo ni mkataba unaokabidhi, kama sio kumilikisha, eneo muhimu la ardhi ya Tanzania kwa nchi nyingine na taasisi zake za kiuchumi kwa muda usiokuwa na ukomo.

Amesema mkataba huo unaovunja uhuru wa nchi na uwezo wake wa kufanya maamuzi yanayohusu maendeleo ya nchi kwenye maeneo yote ya mkataba.

Pia, amesema ni mkataba utakaosababisha unyang'anyi mkubwa wa ardhi dhidi ya wananchi wetu.


"Ni mkataba unaohoji, kama sio kukiuka, misingi muhimu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ni mkataba ambao, kwa maoni yangu, utakuwa msumari wa mwisho katika jeneza la utawala wa CCM katika nchi yetu," amesema Lissu.

Kwa upande mwingine mchambuzi wa sera za umma Bubelwa Kaiza, akizungumza na Mwananchi digital kwa simu, amesema unapoondoa masharti ya umiliki wa ardhi kwa mgeni ni jambo linaloiweka nchi katika hatari kwa kuwa ni rahisi mgeni kuichukua kwa kuzingatia makubaliano yaliyomo kwenye mkataba.

"Serikali imeshindwa kuweka kizingiti chochote kwa DPW iwapo itahitaji ardhi kufanya shughuli zake, hii ni hatari sana. Ni sawa na kuuza ardhi ya nchi," alisema.

Kaiza alisema kwa mantiki hiyo, Serikali itawajibika kutoa ardhi na kutojali wananchi na mali zao kwa kumnufaisha mwekezaji.


"Wanataka kutueleza kuwa mikataba midogo midogo itakayokuja itakuwa na unafuu kwa kuwa haitaweza kutoa ufafanuzi zaidi ya kupinga mkataba mkubwa," amesema.

Naye Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke amesema usuluhishi wa migogoro yote kupelekwa katika baraza la usuluhishi, chini ya sheria za usuluhishi za Kamisheni ya Umoja wa Mataifa juu ya sheria zinazohusika na biashara za kimataifa, ni kinyume cha sheria za nchi zinazoelekeza kufanyika ndani.

Kwa mujibu wa maelekezo ya kifungu cha 11 cha sheria ya mamlaka ya nchi kuhusu umiliki wa rasilimali na maliasili za Tanzania ya mwaka 2017, migogoro ya aina hiyo inatakiwa kutuliwa nchini.

“Kwa hiyo unaweza kupinga mahakamani eneo hilo tu na ukashinda, ukweli bado maswali ni mengi sana,” alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad