Kutoweka kwa nyambizi ya kitalii wakati wa ziara ya kwenda kujionea mabaki ya meli ya Titanic imeibua maswali kuhusu ni hatari gani zinazohusika safari kama hizo kuelekea kilindini.
Wakati fulani katika msimu wa vuli kipande kikubwa cha barafu kilipasuka kutoka kwenye barafu kusini-magharibi mwa Greenland. Kwa muda wa miezi iliyofuata, ilielea polepole kuelekea kusini, ikiyeyuka polepole kufuata mikondo ya bahari na upepo.
Kisha, usiku wa tarehe 14 Aprili 1912, barafu yenye urefu wa mita 125 (410ft) - yote yaliyosalia ya kipande cha barafu kinachokadiriwa kuwa 500m (1,640ft) kilichoacha fjord huko Greenland mwaka uliopita - kiligongana na meli ya abiria ya RMS Titanic ilipokuwa ikifanya safari yake ya kwanza kutoka Southampton nchini Uingereza hadi New York, Marekani.
Ndani ya muda wa chini ya saa tatu meli hiyo ilikuwa imezama, na kuwaangamiza zaidi ya abiria 1,500 na wafanyakazi waliokuwa wameiabiri.
Mabaki ya meli hiyo sasa iko karibu 3.8km (12,500ft) chini ya maji karibu maili 400 (640km) kusini mashariki mwa pwani ya Newfoundland.
Milima ya barafu bado inahatarisha usafiri wa meli - mwaka wa 2019 milima ya barafu 1,515 ilisogezwa kusini hadi kwenye njia za meli zinazovuka Atlantiki wakati wa miezi ya Machi hadi Agosti. Lakini sehemu ilipo mabaki ya meli ya Titanic ina hatari zake, kumaanisha kwamba kutembelea eneo la ajali la meli hiyo maarufu zaidi ya duniani kunaleta changamoto kubwa.