Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imesitisha ratiba za mabasi tisa yaendayo mikoani yanayoanza safari zake kuanzia saa 9:00 alfajiri.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Juni 19, 2023 na Mkurugenzi Mkuu Latra, Habibu Suluo amesema wamefuta ratiba hiyo kwa mabasi sita ya kampuni ya Ally’s Star na matatu ya kampuni ya Katarama Express.
Amesema mabasi hayo sasa yatapaswa kuanza safari saa 12:00 asubuhi kuanzia Jumatano Juni 21,2023 na endapo wataendelea kukiuka maelekezo hayo watafuta leseni zao.
Suluo amesema wamekuwa wakipokea taarifa na wenyewe pia kuthibitisha uwepo wa baadhi ya watoa huduma wa mabasi ynayokwenda mkoani kucheza na mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi na kusababisha kusafiri kwa mwendokasi kwa lengo la kufanya mashindano ya kufika wa kwanza vituo au stendi za mabasi.
Amesema watoa huduma hao wanatuma fursa ya iliyotolewa ya kuanza safari mapema na kufanikisha azma ya kufanya mashindano ya kufika wa kwanza kwenye vituo vya mabasi.
“Takribani wiki mbili sasa kumekuwa na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha mabasi ya Ally’s Star, Katarama Express na Ismamilo yakishindana kufika katika vituo vya mabasi, basi lililoshinda lilimwagiwa maji na kushangiliwa, waliobashiri litawahi walipata ushindi kwenye kamari waliyoicheza kinyume na taratibu.
“LATRA kwa kuzingatia jukumu lake la kukuza usalama wa sekta zinazodhibitiwa ikiwa ni pamoja na usalama wa watumiaji wa huduma za sekta zinazodhibitiwa haiwezi kuacha matendo haya hatari yenye kuhatarisha usalama na Maisha ya watu pamoja na mali zichezewe bila kuchukua hatua stahiki,” amesema