Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR) imempa ushindi Mwanaharakati wa Katiba, Bob Wangwe katika kesi ya kupinga Wakurugenzi wa Halmashauri Kusimamia Uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Katika uamuzi huo ambao umetolewa leo mbele ya Jopo la Majaji Watano, pia Mahakama imeiagiza Serikali ya Tanzania kufanyia marekebisho vifungu vya Sheria ya uchaguzi 7(1) na 7(3).
Akiongea na Ayo Tv, Wangwe amesema “Kimsingi wamekubali kwamba vifungu vya sheria ya uchaguzi 7(1) na 7(3) katika sheria ya Taifa ya Uchaguzi vinavyoruhusu Wakurugenzi kusimamia uchaguzi vinakiuka mkataba wa Mahakama hiyo na mikataba mingine ya ya kimataifa ya haki za Binadamu kwakuwa havijaweka utaratibu wa kuwazuia Watu wenye itikadi za Vyama kutokuwa Wasimamizi wa uchaguzi na hivyo kuathiri ushiriki wa Wananchi katika kushiriki kwenye utawala wa Nchi kwakuwa pia vinaruhusu ubaguzi wa kiitikadi.
"Hivyo Mahakama imeagiza kuwa vifanyiwe marekebisho na Serikali haraka iwezekanavyo na ndani ya miezi 12 ipeleke ripoti ya utekelezaji katika Mahakama hiyo,".
Itakumbukwa kuwa May 24, 2019 Mahakama kuu ilifuta sheria iliyokuwa inawapa Wakurugenzi hao mamlaka ya kuwa Wasimamizi wa uchaguzi lakini Oktoba 17, mwaka huo huo Mahakama ya Rufani ikatengua uamuzi huo.