Ama kwa hakika raia namba moja wa nchi yetu, Rais Samia Suluhu Hassan, au MAMA kama tunavyopenda kumuita, ameongeza chachu na hamasa kubwa kwenye mafanikio ya klabu zetu kimataifa.
Kampeni yake ya bao la mama imepokewa vizuri kuanzia mitaani hadi kwa wachezaji wenyewe. Hili siyo jambo dogo hata kidogo. Kuwafanya watu wote wazungumzie kitu kimoja, ni jambo kubwa kwenye uimara wa kijamii (social stability) na ndicho kitu kinachojenga umoja wa kitaifa.
Haya mamilioni ambayo mama amekuwa akiyamwaga kwa vilabu vyetu, angeweza kupeleka sehemu yoyote na isingekuwa shida kwake.
Lakini kaamua kuyaleta kwenye mpira ili sisi wanaye tufurahi naye mama yetu. Na kweli tumefurahi na tunajivunia sana.
LAKINI
Kwa hali ilivyo sasa, mama inabidi afanye jambo kitofauti…afanye zaidi ya awali, yaani aongeze mzigo. Mama atoe milioni 20 kwa kila mchezaji, siyo tena kwa bao. Na kampeni ibadilike badala ya kuwa bao la mama, iwe ushindi wa taifa.
Hii itaongeza morali kwa wachezaji na kuona kabisa kwamba siyo tu rais yuko nao, bali taifa zima. Yanga wamefungwa nyumbani lakini hayo siyo matokeo ya mwisho. Mashindano ya mechi za mikondo miwili huwa na maajabu yake.
USM Alger walikuwa Dar Es Salaam wakiwa na tahadhari kubwa. Lakini ushindi walioupata unaweza kuwapumbaza na kudhani wamemaliza kazi.
Ile tahadhari waliyokuja nayo itapungua kwa kiasi kikubwa na kujenga kujiamini kupita kawaida. Hapo ndipo Yanga wanaweza kupenyea na kubadili matokeo…amini inawezekana.
Na rekodi zinaonesha kwamba Yanga wamekuwa na matokeo mazuri zaidi ugenini kwenye harakati zao za msimu huu hadi kufika fainali.
Baada ya sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Club Africain ya Tunisia, Yanga walikatiwa tamaa lakini wakaenda kubadili matokeo kule.
Kwenye robo fainali, waliwashangaza Rivers United kutoka Nigeria, katika ardhi yao ya nyumbani. Marumo Gallants ya Afrika Kusini iliugeuza uwanja wao nyumbani kuwa machinjio ya wageni, hadi walipoenda Yanga.
Kwa hiyo Yanga wanao uwezo wa kufanya jambo ugenini…wanaweza kabisa kugeuza matokeo. Kinachotakiwa ni mipango yao ya ndani, lakini sisi huku nje tukiongozwa na raia namba moja, mama yetu Samia Suluhu Hassan, tusiwakatie tamaa.
Ndiyo maana tunasema mama aongeze mzigo…aongeze sifuri kadhaa mbele ya Ile namba mbili. Mwili wa binadamu umeumbwa na homoni za mapambano zinazoitwa Adrenaline. Mara zote anayeshinda vita ni yule aliyeziamsha kwa wingi homoni zake.
Haya mamilioni yatasaidia kuamsha adrenaline za vijana wetu na kuongeza ari ya kupambana uwanjani. Ari ikiongezeka maana yake kupambana kutakuwa kukubwa zaidi na kama itakuwa hivyo maana yake wapinzani watakutana na timu tofauti na waliyokutana nayo Dar Es Salaam.
Kama ambayo Tanzania imelia nyumbani, Algeria nayo inatakiwa kulia kwao…na inawezekana. Makosa madogo madogo ya kiufundi na binafsi yaliyowagharimu Yanga yanaweza kurekebishwa kwenye uwanja wa mazoezi, lakini hamisi ya kitaifa haiendi mazoezini, inapatikana kwa mtindo huu.
Taarifa zinasema uongozi wa Yanga na wadhamini wao wameahidi milioni 63 kwa kila mchezaji. Hizo ni pesa nyingi, lakini pesa huwa hazitoshi…kadri zinavyoongezeka ndivyo zinavyozidi kuhitajika. Kwa hiyo mama afanye jambo…hii ni nafasi pekee ambayo Tanzania imeipatia, tena baada ya miaka 30. Yawezekana nafasi kama hii isirudi tena katika utawala wa mama, kwa hiyo siyo nafasi ya kuiacha ipotee hivi hivi.
Yanga wakichukua Kombe la Shirikisho la CAF, itaandikwa kwenye historia kwamba walichukua wakati mama akiwa madarakani, na alichangia kwa kiasi kikubwa kuongeza hamasa kwa wachezaji na viongozi. Hii ni nafasi ambayo hakuna Rais wa Tanzania aliipata. Hii ni nafasi ambayo Afrika Mashariki imekuja mara tatu tu, ukiacha safari hii.
1987 pale Gor Mahia walipofika fainali ya Kombe la Washindi barani Afrika na kulichukua. Kombe la Washindi ni mashindano ya vilabu barani Afrika yaliyokuwa yalishirikisha mabingwa wa Kombe la FA kutoka nchi zote wanachama wa CAF.
Wakati huo Afrika ilikuwa na mashindano matatu ya ngazi ya vilabu.Klabu Bingwa Afrika – iliyoshirikisha mabingwa wa ligi za kila nchi.Kombe la Washindi – lililoshirikisha Washindi wa Kombe la FA la kila nchi. Kombe la CAF – lililoshirikisha Makamu bingwa, yaani timu zilizoshika nafasi ya pili kwenye ligi za kila nchi. Hili ndilo Kombe ambalo Simba waliingia fainali mwaka 1993, miaka 30 iliyopita. Mwaka 2004, Kombe la Washindi na Kombe la CAF, yaliunganishwa na kuzaliwa Kombe la Shirikisho ambalo Yanga wameingia fainali safari hii.
Ukiacha Gor Mahia, timu nyingine ya Afrika Mashariki iliyokaribia kubeba ubingwa wa Afrika ni Sports Club Villa ya Uganda ambayo ilifika fainali ya klabu Bingwa Afrika 1991.
Kwa hiyo utaona kwamba nafasi hizi na fainali zinakuja kwa nadra sana katika ukanda huu wa Afrika. Ushindi wa Yanga utamfanya mama aandike historia kubwa na ya kipekee. Mama fanya jambo…ongeza mzigo kwa vijana. Milioni 20 kwa kila mchezaji itapendeza!