Kikosi cha ulinzi wa pwani ya Marekani, kimeanzisha uchunguzi kubaini kilichosababisha dhoruba chini ya bahari, ambayo ilipelekea Nyambizi ya Titan kupata ajali na kuuwa watu wote watano waliokuwa ndani ya chombo hicho.
Kikosi hicho, kimesema kitashirikiana na mashirika mengine ya kimataifa, ikiwemo bodi ya usalama wa usafiri ya Canada na tawi la uchunguzi wa ajali za baharini la Uingereza, kuchunguza ajali hiyo iliyotokea Juni 18, 2023.
Jana Juni 25, 2023 Mkuu wa shughuli ya uchunguzi wa kikosi cha walinzi wa pwani cha Marekani, Kapteni Jason Neubauer, alisema operesheni ya kuitoa nyambizi inaendelea na tayari wameshatambua eneo ilikotokea ajali.
Chombo hicho cha Nyambizi ya utalii Titan ilipotea karibu na Meli iliyozama zaidi ya miaka 100 ya Titanic na kulipuka katika kina kirefu cha bahari ikiwa na mvumbuzi Mwingereza Hamish Harding, mtaalamu wa manowari Mfaransa Paul-Henri Nargeolet, tajiri wa Pakistani-Muingereza, Shahzada Dawood na mwanawe Suleman, na Stockton Rush, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni inayoendesha nyambizi hiyo ya OceanGate Expeditions.