Mfanyabiashara adaiwa kuua kwa bastola Himo





Moshi. Ni mauaji yaliyotikisa mji wa kibiashara wa Himo wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro, baada ya mfanyabiashara mashuhuri katika mji huo, Kennedy Minja (47) kudaiwa kumfyatulia risasi na kumuua papo hapo, mkazi wa Kilema, Deogratius Lyimo.

Baada ya tukio hilo, inaelezwa mfanyabiashara huyo aliendesha gari lake umbali wa kilomita 27 kutoka mji wa Himo hadi Moshi mjini ambako inadaiwa alijisalimisha kituo kikuu cha Polisi na hadi leo ana siku 18 anashikiliwa polisi.

Ni tukio lilitikisa mji huo kutokana na umaarufu wa mfanyabiashara huyo wa mazao na namna mauaji hayo yanavyodaiwa kutokea, yakihusishwa na mzozo wa dakika chache baina yake na marehemu.

Wananchi wa mji huo hawaelewi kiini hasa cha mauaji, kama kweli ni baada ya tajiri huyo kuwakosakosa kuwagonga marehemu na ndugu yake waliokuwa na pikipiki au la.

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limethibitisha kumshikilia mfanyabiashara huyo pamoja na bastola anayodaiwa kuitumia katika mauaji hayo na huenda akafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia leo kwa tuhuma za mauaji.

Alipoulizwa jana kuhusu ni lini mfanyabiashara huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani, Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Yahaya Mdogo alisema: "Jalada limeshapelekwa kwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali, ila nafuatilia kujua ni lini atafikishwa mahakamani, huku kukiwa na taarifa huenda akafikishwa mahakamani kesho.

Awali Kamanda wa polisi mkoani hapa, Simon Maigwa alisema tukio hilo lilitokea saa 4:30 usiku wa kuamkia Mei 17, 2023 katika Barabara ya Himo-Marangu ambako mfanyabiashara huyo anadaiwa kumuua Lyimo.


Aliyeshuhudia afunguka

Richard Mahoo, aliyekuwa amempakia Deogratius, wakitokea Himo kuelekea Kilema alidai walipofika karibu na ofisi ya mbunge wa Vunjo, mfanyabiashara huyo aliingia barabarani bila tahadhari na kutaka kuwagonga na gari lake.

Mahoo alidai kitendo kile kilisababisha Deogratius kushuka kwenye pikipiki na kumfuata na kumuuliza kwa nini anataka kuwagonga, lakini mtuhumiwa alishuka kwenye gari na kutamka maneno kuwa, “nyie mlikuwa mnatakaje”. “Kauli ile ilimkera marehemu na kuanza kushikana na kuanza kupigana. Wakati huo mimi nilikuwa naegesha pikipiki vizuri ili niwafuate, kitendo cha mimi kushuka kwenye pikipiki nikasikia mlio wa bastola, nikachanganyikiwa na kukimbia,"alidai.

Aliongeza: "Nilikimbia kama hatua 200 ndipo nikasimama na kuangalia nini kinaendelea, huyo mwenye gari akapiga tena risasi nyingine kunielekezea mimi, lakini haikunipata, ndipo akawasha gari na kukimbia," alidai Mahoo.

Kwa mujibu wa shuhuda huyo, baada ya milio hiyo ya risasi watu walijitokeza na kumchukua marehemu na kumpeleka Hospitali ya Faraja Himo na walipomfikisha waliambiwa ameshafariki dunia.

Kwa upande wa baba mkubwa wa marehemu, Isaack Lyimo alisema kijana wake alitokea kwenye msiba wilayani Siha akiwa na rafiki yake na walipofika Himo, walichukua pikipiki ya huyo rafiki yake kwa ajili ya kuelekea nyumbani Kijiji cha Kyou, Kilema.

Mzazi huyo alidai walipofika jirani na ofisi ya mbunge wa Vunjo kulitokea kuzozana kati ya mfanyabiashara huyo na mtoto wake baada ya mfanyabiashara huyo kuingia barabarani bila tahadhari na kutaka kuwagonga.

Kulingana na maelezo aliyopewa, katika mabishano hayo walifikia hatua ya kutaka kupigana, ndipo mfanyabiashara huyo inadaiwa alikwenda kwenye gari na kuchukua bastola na kumfyatulia risasi mtoto wake na kumuua papo hapo.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad