Mbeya. Mkurugenzi wa Kampuni ya Giant Tanzania Printers Ltd ya jijini Dar es Salaam, Deogratius Magubo amekutwa amekufa kwenye nyumba ya kulala wageni ya Dicco Inn iliyopo eneo la Iyunga Jijini Mbeya.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amewaeleza waandishi wa habari leo Jumatatu, Juni 26, 2023 kuwa mwili wa marehemu ulitambulika Juni 21 saa 5.40 asubuhi baada ya mhudumu wa nyumba hiyo ya wageni kutaka kufanya usafi.
“Marehemu inaelezwa alifika Juni 19 na kupanga chumba namba 208 katika nyumba hiyo ya wageni akitokea jijini Dar es Salaam na Juni 21 polisi walipokea taarifa ya kifo chake huku akiwa amelala ndani ya chumba alichokuwa amepanga ,”amesema.
Amesema awali zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Giant Tanzania Printers Ltd akiwa amelala katika nyumba ya kulala wageni iitwayo Dicco Inn iliyopo maeneo ya Iyunga mkoani Mbeya kwa madai siyo cha kawaida.
Aidha amesema baada ya kupata taarifa katika Kituo Kikuu cha Polisi Mbeya kutoka kwa meneja wa nyumba hiyo ya wageni (jina limehifadhiwa), Mkuu wa Upelelezi wa makosa ya jinai wilaya na uongozi wa Kata ya Iyunga walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili wa marehemu na kuupelekea Hospitali ya Rufaa Kanda kwa uchunguzi zaidi.
“Katika chumba alicholala marehemu kulikutwa dawa mbalimbali za binadamu, ikiwepo Haloxen 1.5, Haloperidol Injection BP, Valparin Chrono 500, Cough Mixer Syrup pamoja na chupa tupu ya pombe aina ya Grants yenye ujazo wa mil 750 na glasi ambalo ndani yake kulikuwa na vipande vitatu vya limao,” amesema Kuzaga.
Amesema uchunguzi wa awali uliofanywa na Jeshi la Polisi katika chumba alichokuwa amepanga marehemu umebaini kuwa hakuna kitu kingine kinachotiliwa mashaka kusababisha kifo chake.
Kamanda Kuzaga amesema Juni 24 mwaka mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi na daktari mtaalamu wa upasuaji katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya mbele ya ndugu wa marehemu kwa kuchukua sampuli na kusafirisha kwa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam kwa uchunguzi zaidi.
Amesema Jeshi la Polisi linasubiri matokeo ya uchunguzi na majibu ya sampuli iliyochukuliwa ili kulinganisha na majibu ya daktari ili kuthibitisha kifo cha Magubo ikilinganishwa na uchunguzi wa awali uliopatikana kwenye chumba alichokuwa amepanga.
Kamanda Kuzaga amewaomba wananchi kutoa taarifa zinazohusiana na tukio hilo licha ya kuwepo kwa uchunguzi inaendelea kufanywa wa kisayansi kujua sababu ya kifo chake.
Mwananchi