Mwanafunzi Chuo cha Ushirika Afariki Dunia Akiogelea

Mwanafunzi Chuo cha Ushirika Afariki Dunia Akiogelea
 

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Holence Rwazo amefariki dunia kwa ajali ya maji, wakati akiogelea katika chemchem ya maji moto iliyoko Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa, lilitokea juni 24, mwaka huu, wakati mwanafunzi huyo ambaye alikuwa akisoma Shahada ya Masoko na Ujasiriamali,  akiogelea kwenye chemchem hiyo na kwamba chanzo cha tukio hilo ni marehemu kuzidiwa na maji wakati akiogelea.



"Juni 24, saa 6:00 mchana huko Kijiji cha Chemka Kata ya Masama Rundugai, Hassan Fumbwee mkazi wa Njiapanda ya KCMC aligundua kufariki kwa rafiki yake Holence Rwazo mwanafunzi wa Chuo cha Ushirika Moshi kozi ya masoko na ujasiriamali mwaka wa tatu wakati wakiogelea kwenye chemchem ya maji moto Chemka," amesema.


Akizungumzia kifo hicho, Ofisa Mawasiliano na Masoko Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Fadhila Erick amesema mwanafunzi huyo alipata ajali hiyo wakati akiwa kwenye matembezi binafsi.


"Alifariki kwa ajali ya maji katika chemchem ya chemka ambapo alienda kwenye matembezi binafsi, chuo tumepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa kifo hiki," amesema.


Baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho, Jesca Amon na Exaud Singano wamesema kifo hicho kimewashtua kwa kuwa kimekuwa cha ghafla.


"Kifo cha mwanafunzi mwenzetu kilitushtua maana ilikuwa ni ghafla na alikuwa anakaribia kumaliza chuo ni huzuni kwani tumempoteza kijana mwenzetu ambaye bado alikuwa akitegemewa na Taifa," amesema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad