Dodoma. Mbunge wa Ngara (CCM), Ndaisaba Ruhoro anadaiwa kulazimisha picha zake zibandikwe maeneo yenye mkusanyiko wa watu ndani ya jimbo huku baadhi ya watu wakihoji kwa nini iwe lazima.
Picha hizo zinaelezwa kubandikwa maeneo ambako kuna picha za Rais na sehemu ambazo hakuna picha za kiongozi mkuu wa nchi kwa madai yeye ndiye kiongozi wa Ngara.
Mbunge huyo amekiri kuwepo na picha zake nyingi maeneo tofauti zikiwemo nyumba za watu na kutaja sababu kuwa inatokana na mapenzi waliyonayo wananchi kwake, hivyo haoni kosa kwa watu kufanya hivyo.
Ruhoro analalamikiwa kulazimisha wenye maduka, migahawa, saluni na taasisi nyingine kuwa na picha zake ilihali maeneo mengi yamebandikwa picha za Rais na viongozi wa juu.
Katika maeneo mengi ya Ngara ambayo gazeti hili lilipita, picha za mbunge huyo zinaonekana kupamba maduka na maeneo yenye mikusanyiko kwa kuwekwa kwenye vioo kama ilivyo kwa picha za Rais na kutundikwa kwenye kuta kama ishara ya kiongozi wa eneo husika.
Mmoja wa wafanyabiashara wa maduka mjini Ngara alikiri kwenye maduka yake mawili ameweka picha za mbunge huyo, lakini akaeleza kuwa si kwa utashi wake, bali anasukumwa na biashara yake.
“Sijazungumza na Ruhoro mwenyewe kuhusu hili, lakini wapambe wake wanaleta picha kwamba lazima ubandike kwenye eneo la wazi na bila kufanya hivyo usije kulaumu. Ndugu yangu utafanyaje kama ni wewe maana hawa ndiyo waamuzi wa kila kitu. Wananchi tunataka maendeleo sio kulazimishwa kubandika picha za wanasiasa kwenye biashara zetu,” alisema mfanyabiashara huyo ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.
Kwa mujibu wa mfanyabiashara huyo, picha za mbunge zinatengenezewa Ngara hakuna malipo kwa mmiliki wa ofisi zinapobandikwa, jambo ambalo linawakwaza zaidi.
Baadhi ya wananchi walisema kwa sasa picha hizo zinasambazwa vijijini hasa maeneo yaliyochangamka na mtindo ni ule ule wa wahusika kulazimisha picha ya mbunge huyo kuwekwa eneo la wazi.
Mmiliki wa studio inayozalisha picha hizo Dedu Production, Juma Dedu alisema hafahamu zinakwenda kutumika kwa matumizi gani na hajafuatilia kama zinasambazwa kwa lazima kama inavyodaiwa.
Dedu alisema kazi wanazofanya kwenye studio hiyo ni kusafisha na kuzalisha picha na ni biashara kama zilivyo nyingine, hivyo hawezi kuzuia kama kuna watu au mtu anataka kuzalisha picha ilimradi amlipe fedha. “Nafanya biashara, ukiniuliza kama nazalisha picha za mbunge jibu langu ndiyo lakini si yeye, mbona kuna watu wanazalisha picha nyingi sana je nao tuseme wanapeleka wapi?” alihoji.
Alipoulizwa nani anazilipia picha hizo gharama za kuzidulufu, alisema si kazi yake kumkariri mtu mmoja kila siku badala yake anajua kuwa hakuna mahali anadai fedha kuhusu kazi hiyo.
Akitoa ufafanuzi wa picha hizo kusambazwa jimboni, Ruhoro alisema hakuna shida wala kosa, kwani wanaozisambaza ni wananchi wenyewe kwa mapenzi yao.
Alisema hatoi hata shilingi yake mfukoni kugharamia picha hizo isipokuwa wanaompenda ndiyo huzichapisha na kuweka maeneo mengine.
Hata hivyo, alisema kuna watu wanaoogopa kivuli chake ndiyo wanalalamikia hilo akimtuhumu mmoja wa wastaafu anayedai anataka kugombea, lakini anakuwa na hofu.
“Tafuteni mambo ya Nikel na vitu vingine muandike, siasa za Ngara zina mambo mengi kama wanaogopa picha zangu nikifika majukwaani si watakimbia, kesho tena utasikia mbunge kampa mimba mtu mara hazai hao wanaweweseka,” alisema.
Alisema kwa upande wake haoni shida kwa sababu picha zake zimeandikwa ni mbunge cheo ambacho ni halali, lakini hajaandika Rais, Makamu au Waziri Mkuu.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngara, Vitari Ndairagije alisema taarifa za kusambazwa kwa picha hizo hajazipata, hivyo hawezi kutoa maoni yoyote kwa sasa