Shekhe Ponda Issa Ponda
KATIBU wa Shura ya Maimamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, ameipongeza Serikali kwa kuupeleka bungeni jijini Dodoma, mkataba wa ushirikiano wa kiserikali kwa ajili ya uendeshaji Bandari nchini kati yake na Serikali ya Dubai, kwa ajili ya kujadiliwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Akizungumza na waandishi wa habari, jana Alhamisi, jijini Dar es Salaam, Sheikh Ponda amesema suala hilo ni la kupongezwa kwa madai kuna baadhi ya mikataba nyeti iliwahi kupitishwa bila kujadiliwa na mhimili huo.
Amesema kitendo cha Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuupeleka bungeni mkataba huo wa ushirikiano kati yake na Kampuni ya DP World ya Dubai, umerejesha uhai na heshima ya Bunge.
“Katika suala hili tusirudie makosa ya nyuma, tujikumbushe jinsi katiba ilivyovunjwa mara kadhaa na Serikali kwa kuingia mikataba mikubwa na wawekezaji, hasa wazungu bila kuipeleka bungeni ikajadiliwe kama sheria inavyoagiza,” amesema Sheikh Ponda.
Ametaja baadhi ya mikataba ambayo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. John Magufuli iliingia na wawekezaji bila kuipeleka bungeni ikiwemo ya madini iliyoingia kati ya Tanzania na Barick Gold Corporation.
Mikataba mingine ni wa kuchimba madini ya Nickel kati ya Tanzania na Kampuni ya ZL Nickel kutoka Uingereza na mkataba wa ujenzi wa bomba la mafuta kati ya Tanzania na Uganda.
“Mikataba hii tisa kati ya Tanzania na Barick baada ya mgogoro wa kodi kati ya Tanzania na Kampuni ya Acacia ambayo ni baba yake Barick. Hawa Barick wanaendesha migodi mikubwa ya dhahabu ya Buzwagi, North Mara na Bulyanhulu. Serikali haikuona umuhimu wa mikataba nyeti kwenye rasilimali ya Taifa kupelekwa kwa wawakilishi wa wananchi bungeni ukajadiliwe,” amesema Sheikh Ponda.
Aidha, Sheikh Ponda, ameshauri mkataba wa ushirikiano wa kiserikali wa kuendesha bandari nchini kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai, uboreshwe kama inavyopendekezwa na wananchi.
Katika hatua nyingine, Sheikh Ponda ametaka mjadala kuhusu uboreshaji mkataba huo, ujikite katika kuleta ufanisi wa uendeshaji bandari, badala ya udini, utanganyika na uzanzibar, kama inavyofanywa na baadhi ya watu.
Sheikh Ponda ameunga mkono uamuzi wa Serikali kutafuta muwekezaji katika sekta hiyo, akisema bandari zinapaswa kuboresha Ili kuongeza ufanisi wake kwa ajili ya kujipatia nchi mapato.
Amesema watalamu wa uchumi wanaeleza zinaweza kulipa watumishi wa umma na deni la Taifa, endapo zitatumika vizuri.
Sheikh Ponda amesema kwa Sasa Bandari zinakosa mapato kutoka katika shehena za mizigo ikiwemo madini kutoka Congo na Uganda, ambapo nchi hizo hutumia Bandari kavu ya Rwanda, inayoendeshwa na DP World, kusafirisha.
Ambayo haina sifa ya kijiografia kwa kuwa Iko mbali ukilinganisha na Bandari ya Dar es Salaam.
Sheikh Ponda amesema kuna baadhi ya taasisi, mashirika, viwanda na biashara zilikuwa zinafanya vizuri kabla ya Tanganyika Kupata uhuru, lakini zilifilisika baada ya kutaifishwa na Serikali.
Baadhi ya mashirika hayo ni Kiwanda cha Nguo Cha Musoma (MUTEX) na Kiwanda Cha matairi ya magari (General Tire).
“Tabia ya Watanzania kung’ang’ania kumiliki au kuendesha jambo hata kama hawaliwezi na halina faida kwao linawaumiza . Katika mjadala uliopo wa DP World ya Dubai waendeshe Bandari ya Dar es Salaam au tusiwape yupo kiongozi wa dini alisema tusiwape Bali tuwajengee uwezo watu wetu. Bila shaka historia fupi ya uchumi wa Tanzania tuliyoitoa hapo inaweza kitusaidia katika hoja hiyo.