MFANYABISHARA wa Kimataifa ambaye pia ni mwanasiasa, Rostam Aziz amejibu Balozi Dk. Wilbrod Slaa ambaye alimtuhumu kwa mambo mbalimbali na kusisitiza kwamba Katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema ni kizabizabina. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).
Rostam ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Juni 2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwekezaji wa Kampuni ya ya Taifa Gesi nchini Zambia.
Aidha, akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu tuhuma zilizotolewa hivi karibuni na Balozi Dk. Wilbrod Slaa kwamba anahusika na uwekezaji huo, Rostam amesema hana uadilifu wala uaminifu wa kumsema.
“Dk. Slaa sijui nimjibu nini maana historia yake haimpi heshima wala uhalali kujifanya eti yeye ni mtu wa kujali masilahi ya Mtanzania, siku zote amejijali yeye binafsi na masilahi yake binafsi.
“Tujikumbushe historia yake na rekodi yake kwamba ni mtu ambaye aliacha kazi ya utumishi wa Mungu kanisani baada ya utovu wa maadili na kuona maisha yake binafsi ni bora kuliko utumishi wa Mungu.
“Ni historia ya kukosa uaminifu na uadilifu, pia watanzania wajikumbushe historia yake na rekodi yake ya mwaka 1995 kwamba hakujiunga na upinzani kwa sababu ya imani yake, bali ni kwa sababu jina lake lilikatwa alipogombea kupitia CCM na sababu iliyotolewa ni kukosa uadilifu alipokuwa akifanya kazi ya utumishi wa Mungu,” amesema.
…ALIHONGWA KUISALITI CHADEMA
Rostam ameendelea kumuanika Dk. Slaa na kuwakumbusha Watanzania kuhusu uchaguzi wa mwaka 2015 kwa kubainisha wazi kuwa alihongwa ili akisaliti Chadema.
“Huyu mtu alipokuwa Chadema mwaka 2015 aliamua kusaliti chama chake baada ya kuhongwa, akakiasi chama chake, akakaa hoteli ya Serena baadae akaenda Canada na baadae kupewa ubalozi, sasa mtu ambaye hana msimamo, mbinafsi anaangalia masilahi yake hajawahi kusaidia chochote katika uchumi kazi yake kupigapiga tu maneno ni mtu ambaye kumjibu unapata shida ila inabidi kumjibu.
“Hana uadilifu wala uaminifu wa kunisema, historia yake ni tosha kabisa kwamba huyu mtu yuko tayari kupandikiza chuki, uhasama kwa ajili ya masilahi yake binafsi, kwa Kiswahili kifupi huyu bwana ni ‘kizabizabina.
“… mfitini, mbinafsi yupo tayari kusema chochote lolote kwa masilahi yake binafsi. Nadhani huyu ni mtu wa kuogopwa kama ukoma, niwahisi Watanzania kuangalia historia ndipo tuamue anatakiwa kusikilizwa au lah,” alisisitiza Rostam.