Wakati Taarifa za kutakiwa Afrika ua Kusini zikizidi kusambaa na taarifa za uhakika zikidai kuwa wakati wowote Kaizer Chiefs inaweza kumtangaza kocha wao mpya Nasreddine Nabi ambaye wamempa nafasi mbili pekee za kuwaleta watu wake atakaoungana nao kwenye benchi lake jipya.
Ingawa anafanya siri, lakini ni wazi kwamba ataenda na wasaidizi wake wawili kocha wa mazoezi ya viungo Helmy Gueldich na mtaalam wa kuchambua mechi za wapinzani Khalil Ben Youssef ambao wote alitua nao Yanga kwa nyakati tofauti.
Taarifa kutoka nchini Afrika Kusini ni kwamba Nabi ameshinda vita ya kwanza kwa kuishinikiza klabu hiyo kuachana na kocha wao wa viungo Muzi Maluleke ambaye alikuwa bado ana mkataba na Chiefs, lakini amefeli kuondoka na Cedrick Kaze ambaye alikuwa kwenye listi yake.
Nabi aliwapa sharti hilo Chiefs akitaka atue na Helmy ambaye kitaaluma ni Profesa kwa ajili ya mazoezi ya viungo kitu ambacho Wasauzi hao wamekubaliana nalo kwa mbinde wakimlipa msauzi huyo gharama za kumsitishia mkataba.
Mbali na Helmy pia Chiefs imeachana na kocha mwingine ambaye alikuwa akifanya kazi kama mtaalamu wa kuchambua mikanda ya wapinzani kisha kumuingiza ndani Khalil ambaye amedumu Yanga kwa miezi michache tangu ajiunge wakati wa mechi za hatua ya makundi za Kombe la Shirikisho Afrika.
Habari njema kwa Yanga ni kwamba kocha wao msaidizi Cedric Kaze anaweza kusalia kufuatia kushindwa kuondoka na Nabi ambapo Yanga inaweza kumuunganisha na kocha wao anayekuja kumsaidia kumpa taarifa za msingi za kikosi chao.
Kaze amefanya kazi na Nabi kwa miaka miwili akimtangulia Mtunisia huyo ambapo kubaki kwake kunaweza kuwa kitu bora kwa Yanga kwa kuwa anakijua kikosi hicho kwa undani akiwa sehemu nzima ya mafanikio hayo ya miaka miwili.
Yanga pia mbali na vikao vya kumsaka kocha mpya Mwanaspoti linafahamu pia wameshaanza kusaka mrithi wa Helmy na kocha wa makipa baada ya Mbrazil Milton Nienov naye kutimka ikitajwa anakwenda kujiunga na klabu moja nchini kwao akiwa kama kocha mkuu wala si kweli kuwa anageukia Msimbazi.