Dodoma. Wakati Serikali mkazo juu ya zuio la wanafunzi chini ya darasa la tano kusoma bweni, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga wako hatua za mwisho kukamilisha vigezo vitakavyotumiwa na kamishna wa Elimu katika kutoa kibali maalumu.
Kipanga amesema hayo leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Vitimaalum (CCM) Judith Kapinga ambaye amehoji mkakati gani umewekwa wa kudhibiti watoto chini ya miaka saba kusomo shule za bweni.
Akijibu swali hilo, Kipanga amesema Serikali iliandaa mwongozo wa uanzishaji na usajili wa shule uliotolewa Novemba, 2020 ambao umeelekeza juu ya utolewaji wa kibali maalum.
“Mwongozo huo umeelekeza bayana kuwa kibali cha kutoa huduma ya kulaza wanafunzi wa bweni kitatolewa kuanzia darasa la tano na kuendelea,” amesema.
Aidha, Kipanga amesema huduma ya bweni itatolewa kwa kibali maalumu kwa wanafunzi wanaosoma chini ya darasa la tano.
Amesema pia pamoja na kutolewa kwa mwongozo huo, pia, Serikali imetoa waraka wa elimu namba mbili wa mwaka 2023 unawaelekeza wamiliki wa shule wasiokuwa na kibali maalumu cha kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi walio chini ya darasa la tano wasiendelee kutoa huduma hiyo.
Aidha, amesema kwa kushirikiana na wadau wa elimu, wizara inakamilisha kuandaa vigezo vitakavyotumiwa na Kamishna wa Elimu katika kutoa kibali maalumu kwa wananfunzi hao chini ya darasa la tano.
Amesema Serikali itaendelea kudhibiti tatizo la watoto chini ya darasa la tano kusoma shule za bweni kwa kuhakikisha kuwa inafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara.
Kipanga amesema shule itakayobainika kukiuka maelekezo hayo itachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria ikiwemo kufutiwa usajili.