Shafih Dauda Awatetea Wachezaji Wanaoachwa Bila Kupewa Muda wa Kuonyesha Uwezo wao "Hata Chama Alipewa Nafasi"


Klabu za Ligi Kuu zinaendelea kuwatema wachezaji kuelekea msimu ujao, hadi sasa wachezaji walioachwa Simba [7], Coastal Union [6], Azam FC [6], Yanga [4]. Hizo ni baadhi ya klabu ambazo zimetangaza.

Mimi sitegemei klabu isajili wachezaji 10 au zaidi halafu wote kwa pamoja waipe matokeo ndani ya msimu huohuo, kuna ambao wanaweza ku-click lakini kuna ambao watahitaji muda ili kuingia kwenye timu huku wakizoea mazingira mapya, tamaduni, falsafa na aina ya uchezaji wa timu.

Mfano mzuri ni huyu Clatous Chama, alipofika Simba hakuanza kufanya vizuri moja kwa moja kama ambavyo tunamuona leo! Hata Miquossone alipofika alipata muda kidogo wa kuzoea wakati huo Kichuya akiwa wa moto.

Wakati mwingine presha ya mashabiki wa Simba au Yanga inapelekea viongozi kuvunja mikataba hata ya wachezaji ambao pengine wangekuja kuwa msaada kwa timu baada ya muda fulani.

Kwa mfano mchezaji kama Sawadogo au Doumbia wanaweza kuachwa kwa sababu ya presha ya nje, kiuhalisia bado hawajapata nafasi ya kutosha ya kufanya wahukumiwe kwamba wameshindwa!

Wachezaji kama hawa wanahitaji kupata nafasi ya kwenda pre-season warudi wapate nafasi ya kutosha kucheza. Sawadogo alikotoka alikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, kaja Simba kapata majeraha, unamhukunu vipi kuwa kashindwa.

Hawa viongozi wa hizi timu wakati mwingine nawaelewa kwa sababu wana presha ya mashabiki nyuma yao.

Lakini suala la kuacha wachezaji wengi na kusajili wachezaji wengi wapya halina afya kwa sababu katika hao wapya waliosajiliwa sio wote wataanza vizuri, wapo ambao watahitaji muda pengine msimu mzima.

Timu ikichukua ubingwa ndio inakua ngao ya kufunika mapungufu mengine, isipochukua ubingwa presha ipo palepale! Je, mnatimua tena wachezaji na kusajili wengine?

Unamkumbuka Vincent Bossou ilimchukua muda gani kufanya vizuri Yanga? Hata Joyce Lomalisa kuna wakati watu walimbeza wakati hapati nafasi, lakini baadae kila kitu kikabadilika!

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad