Shule Zinazosomesha Wanafunzi Wakati wa Likizo Zaonywa Vikali


Dar es Salaam. Serikali imehimiza viongozi na wakuu wa shule nchini kuwaacha wanafunzi wapumzike pale kipindi cha likizo kinapofika kwani wanahaki yao kuwa na familia zao nyakati hizo.

Katika barua yake kwenda kwa wadau mbalimbali wa elimu, Kamishna wa Elimu Dk Lyabwene Mtahabwa imesema kumejitokeza tabia ya baadhi ya viongozi wa elimu kuendesha shule kinyume cha sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo.

Amesema moja ya tabia hizo ni kuwazuia wanafunzi kwenda likizo mara baada ya shule kufungwa kwa lengo la kuongeza ufaulu katika shule husika.

“Sasa hivi kumezuka wimbi la shule kuwanyima watoto likizo ili wakae shuleni kujiandaa na mitihani. Lililo baya zaidi wazazi wanalazimishwa, dhidi ya matakwa yao kuwaacha watoto wabaki shuleni wakati wa likizo na mara nyingi wametakiwa kulipa gharama za ziada kwa ajili hii,” amesema.

“Napenda kuwakumbusha wamiliki na waendeshaji wa shule kwamba watoto wanayo haki ya kupewa likizo ya kurudi majumbani kwao mara muhula wa masomo unapoisha,” imeeleza barua hiyo.

Vilevile Dk Mtahabwa amesema anahimiza shule ziwape watoto likizo aidha ofisi yake inafuatilia kwa karibu suala hilo na ikilazimika itachukua hatua stahiki kwa sababu watoto wana haki ya kupumzika na kujumuika na familia zao nyakati za likizo.

“Kwa barua hii wamiliki wa shule zote za awali, msingi, na sekondari mnaelekezwa kuhakikisha shule mnazosimamia zinafungwa kwa mujibu wa kalenda ya mihula ya mwaka 2023 na watoto wote wanaondoka shuleni kwenda nyumbani kwa mapumziko na kurejea shuleni kulingana na Kalenda husika.”
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad