Clatous Chama |
Muda wowote kuanzia leo, Simba itaanza mazugumzo rasmi ya kumuongezea mkataba mwingine wa miaka miwili, kiungo wake mshambuliaji Mzambia, Clatous Chama ya kuendelea kubakia hapo.
Hiyo ni baada ya mkataba wa kiungo huyo kubakia wa mwaka mmoja wa kuendelea kuwepo kuendelea kuichezea Simba iliyopanga kukiboresha kikosi hicho kuelekea msimu ujao.
Chama mara kadhaa amekuwa akihusishwa na baadhi ya klabu kumuhitaji za hapa nyumbani za Yanga na Azam FC inayoendelea na usajili wa kufuru kimyakimya ambayo hivi karibuni ilifanikiwa kumnasa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya uongozi wa timu hiyo, Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, upo katika hatua za mwisho za kumuongezea mkataba huo mpya utakaofikia kikomo mwaka 2026.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa kiungo huyo amekubali kuongeza mkataba baada ya vikao kadhaa walivyokaa Bodi ya Wakurugenzi na wote kufikia muafaka wa kutimiza ofa ya Chama aliyoiweka mezani.
Aliongeza kuwa Chama mwenyewe ana tatizo lolote kuongeza mkataba mpya, lakini kikubwa anachokiangalia ni maslahi pekee.
“Simba ipo katika muafaka wa mwisho wa kufikia makubaliano ya kumuongezea mkataba Chama wenye thamani kubwa ambayo ni siri kati ya uongozi na mchezaji mwenyewe.
“Mkataba huo atausaini haraka ndani ya wiki hizi mbili au kabla ya kuanza maandalizi ya Super Cup League yatakayoanza mapema Agosti, mwaka huu.
“Kikubwa Simba haitaki kuwapoteza wachezaji muhimu waliokuwa muhimu katika kikosi cha kwanza, hivyo Chama ni kati ya wachezaji watakaobakia kwa muda mrefu,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alizungumzia hilo la usajili kwa kusema: “Tunajua tunachokifanya katika usajili wetu wa msimu ujao, tumepanga kufanya maboresho makubwa ya kikosi chetu kwa kusajili wachezaji wote ambao wamependekezwa na kocha wetu.”