Simba Yasign Wachezaji Watatu Fasta, Kocha Robertinho Achekelea


SIMBA juzi usiku liliingia dili tamu litakalowapa Sh 4 Bilioni kutoka kampuni ya Sandaland ili kutengeneza na kusambaza jezi za klabu hiyo, lakini kitu kitamu zaidi kwa mashabiki wa klabu hiyo ni taarifa ya kusainiwa kwa mastaa watatu wapya, jambo lililomuibua kocha wa timu hiyo akiwa Brazili.


Simba iliyomaliza misimu miwili mfululizo bila kutwaa taji lolote, ilisaini dili la miaka miwili na Sandaland inayochukua nafasi ya Vunja Bei iliyomaliza mkataba, huku ikiwa na mikakati ya kurejea msimu ujao ikiwa ya moto ili kurudisha heshima iliyokuwa nao misimu minne iliyopita.

Moja ya mikakati ya klabu hiyo chini ya kocha Roberto Oliveira 'Robertinho' ni kusajili mashine mpya zitakazoiongezea nguvu kikosi cha sasa ambacho baadhi ya nyota wake wameanza kupewa mkono wa kwaheri akiwamo Mghana Augustine Okrah na beki Joash Onyango.

Katika kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa, inaelezwa Simba tayari imeshasajili wachezaji watatu ambao ni mapendekezo ya kocha huyo raia wa Brazili ambaye aliliambia Mwanaspoti ana furaha kuona mabosi wa klabu hiyo wanatekeleza kile alichokubaliana nacho wakati anaondoka nchini.


Robertinho alisema licha ya kuwa mapumzikoni, lakini amekuwa akijulishwa kila kinachoendelea kwenye usajili wa Simba, ikiwamo kusajiliwa kwa wachezaji watatu akiwamo winga mkali aliyekuwa akimpigia hesabu kwa muda mrefu, beki wa kushoto na kiungo mshambuliaji.

"Hadi sasa tayari kuna wachezaji kama watatu waliokwisha kusajiliwa na wote ni sehemu ya mipango yangu na nimefurahishwa kwa jambo hili, naamini hadi kumalizika kwa orodha niliyoiitoa kwenye ripoti yangu nitakuwa na timu ya kibabe mno kwa msimu ujao," alisema Robertinho bila kuweka bayana majina ya wachezaji hao watatu waliosaini hadi sasa.

Hata hivyo, Mwanaspoti lilipenyezewa mapema winga aliyekuwa akihitajiwa mno na Mbrazili huyo ni Leandre Onana kutoka Cameroon anayekipigia nchi ya Rwanda, sambamba na beki wa kushoto, Yahya Mbegu, huku klabu hiyo ikiwa imetuma maombi ya kumsajili Milton Karisa wa Vipers ya Uganda, pia ikielezwa inamnyemelea kiungo fundi wa mpira wa Mbeya City, Hassan Nassor 'Machezo' anayewaniwa pia na Singida Fountain Gate (zamani Singida BIg Stars).

Kocha Robertinho alisema kwa kujiamini kwamba 'yajayo' ni utamu zaidi kwani, mikakati ya benchi la ufundi likishirikiana na uongozi mzima wa Simba ni kutaka kuhakikisha msimu ujao mataji yaliyotowekwa kwa misimu miwili yakishikiliwa na Yanga yanarejea klabuni hapo.

"Kazi haijaisha, naamini hadi nitakaporejea kila kitu kitakuwa kimekamilika na kuanza mikakati ya msimu mpya sambamba na michuano ya CAF Super League, ila hadi sasa tupo vizuri kwani naona timu inaenda kubalanzi kama anilivyotaka kwa kusainishwa kwa wachezaji hao wa awali," alisema.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad