YANGA ipo katika hatua nzuri za kukamilisha dili la usajili wa kiungo mkabaji mwenye uwezo wa kuanzisha mashambulizi, Mohamed Zoungrana raia wa Ivory Coast anayekipiga ASEC Mimosas ya nchini huko.
Timu hiyo, hivi sasa ipo katika mipango ya kukisuka kikosi chake ili kifanye vema msimu ujao ambao wanatetea mataji matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho la Azam Sports.
Kiungo huyo anayecheza box to box, ni kati ya viungo waliopo katika mipango ya kusajiliwa na Yanga msimu ujao ambaye anakuja kuchukua nafasi ya Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Chanzo cha habari kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, kimeliambia Spoti Xtra kuwa, tayari mazungumzo yameanza kufanyika kati ya klabu hizo mbili ili kukamilisha usajili huo unaokwenda kuvunja rekodi.
Kilisema kuwa, menejimenti ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye ana uwezo kunyang’anya mipira tayari imeiruhusu Yanga kuanza mazungumzo na Zoungrana aliyebakisha mkataba wa mwaka mmoja ASEC Mimosas.
Kiliongeza kuwa, dili hilo limepangwa kukamilika hadi kufikia Juni 30, mwaka huu mara baada ya Yanga kupewa ofa ya dau la kumsajili nyota huyo.
“Tayari mazungumzo kati ya Yanga na ASEC Mimosas yameshafanyika juu ya makubalino ya ada ya usajili wa kiungo mkabaji Zoungrana anayecheza nafasi hiyo box to box.
“Kiungo huyo ndiye anakuja kuwa mbadala wa Fei Toto aliyeandaliwa jezi namba 6 ambayo ndiyo atakayoivaa katika msimu ujao mara baada ya dili lake kukamilika.
“Uongozi wa ASEC Mimosas umekubali kuwaruhusu Yanga kuanza mazungumzo na menejimenti ya mchezaji, nayo imeitaka Yanga kuwasilisha ofa yao.
“Uongozi wa Yanga kuanzia wiki hii rasmi wataanza mazungumzo na menejimenti ya mchezaji ambayo inamsimamia kwa sasa,” kilisema chanzo hicho.
Yanga kupitia Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ally Kamwe, mara kadhaa kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii amekuwa akitamba kuwa jezi namba 6 itavaliwa na kiungo wa kiwango cha juu ambaye muda wowote atatambulishwa mara baada ya dili lake kukamilika.
STORI NA WILBERT MOLANDI, SPOTI XTRA