UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kwani Fiston Mayele ni nani?

 

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Kwani Fiston Mayele ni nani?

Nilikuwa namtazama Fiston Mayele katika mechi ya DR Congo mjini Kinshasa dhidi ya Gabon Jumapili usiku. Mayele alifunga moja ya yale mabao yake bora ya kutisha ambayo huyafunga mara zote.


Mwanzoni tulidhani makipa na mabeki katika ligi hawafanyi vizuri kumzuia hadi alipoyahamishia katika mashindano ya kimataifa. Bao lake la Jumapili alifunga kutoka katika ule upande wake pendwa wa kushoto ambao huutumia kuwaumiza mabeki na kuwatesa makipa anapopata nafasi ya kushambulia kutoka upande huo.


Mayele anapokuwa kushoto hukimbia kwa kasi kulishambulia sanduku la mpinzani huku akitafuta nafasi ya kupiga kwa mguu wake wa kulia. Anapokosa nafasi ya kukimbia basi hupunguza mabeki kwa chenga na kuweka mpira katika mguu wa kulia kisha kufunga.


Bao lake hilo alifanya yote mawili kwa pamoja. Alikimbia na kumpunguza beki mmoja kisha akazisaka nyavu za Gabon kwa umaridadi mkubwa. Kwani Mayele ni mshambuliaji wa aina gani kwako? Niandikie maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.


Ni mara chache sana kumkuta mshambuliaji anajishughulisha kushoto na kulia mwa uwanja kama anavyofanya Mayele. Ni mara chache sana kumkuta mshambuliaji anayeweza kuwashughulisha mabeki kama Mayele.


Washambuliaji wengi wa mwisho husubiri katika nafasi na kujaribu kufunga, wengi hawajihusishi sana na mchezo. Tazama hata washambuliaji waliotamba miaka ya karibuni nchini kuanzia Amisi Tambwe, Donald Ngoma, Meddie Kagere, John Bocco na sasa Jean Baleke wote ni wazuri katika kufunga lakini si kujihusisha na mchezo. Tafsiri rahisi na ya haraka ni kwamba washambuliaji wanaojihusisha na mchezo na kufunga kama Mayele hawapatikani kirahisi haswa katika Bara la Afrika ambalo washambuliaji wake mahiri wanakimbilia Ulaya na kwa waarabu wa Asia.


Ni bahati kubwa sana kuwa na mshambuliaji kama Mayele kwenye timu yako. Ukiwatazama Yanga tangu usajili wa dirisha dogo wamefanikiwa kuwatumia washambuliaji wao wawili mahiri kwa pamoja, Mayele na Kenedy Musonda kwasababu ya huu uwezo wa Mayele kujihusisha na mchezo zaidi.


Yanga wanaposhambulia Musonda hujitega katikati huku Mayele akikimbia pembeni kutafuta mpira. Unapompoteza Mayele hupotezi mabao yake pekee. Unapoteza mabao na msingi mzima wa uchezaji wa timu. Sielewi ni kwa jinsi gani Yanga wanaweza kumchezesha Musonda na mshambuliaji mwingine ambae sio Mayele.


Kwani Mayele ni Mshambuliaji wa aina gani kwako? Niandikie maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.


Lipo hili lingine. Watu wengi hudai kwamba Mayele hufunga kwa jitihada binafsi zaidi akiwa Yanga. Madai ni kwamba Yanga hawamsaidii kufunga. Yanga hawatengenezi nafasi nyingi za kumfanya mshambuliaji wao mahiri kufunga kwa urahisi.


Uliwaona DR Congo juzi? Hadi Mayele anaingia uwanjani Congo walikuwa na shuti moja pekee lililolenga lango ambalo lilikuwa bao lao lililotoka katika mpira wa kona ambayo Gabon walisinzia kuizuia.


Hawakuwa na nafasi nzuri za kufunga walizowatengenezea washambuliaji wao. Ilibidi wamsubiri Mayele atoke benchi kuja kujitengenezea nafasi ya pili na ya bao katika mechi ambayo ilikuwa inaonekana kuwazidi nguvu. Unapokuwa na Mayele unakuwa na uhakika wa bao hata kama timu haitengenezi nafasi.


Wapo washambuliaji wachache sana barani wanaomzidi Mayele kwa sasa, sizifahamu timu nyingi Afrika ambazo zinaweza kumuweka nje Mayele. Hata wakati kocha wa DR Congo anahitaji kufanya mabadiliko alilazimika kumgeukia Mayele na kumuacha Makabi Lilepo ambae alifunga sana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na Al Hilal ya Sudan.


Unadhani alibahatisha kumchagua Mayele badala ya Lilepo? Hapana! Ukweli ni kwamba Mayele ni mshambuliaji hatari sana kwa sasa. Pengine haanzi DR Congo kwa sababu wanaocheza katika nafasi yake wanatoka Ulaya.


Kibonzo zaidi cha bao la Mayele katika mchezo dhidi ya Gabon kilikuwa pale ambapo wachezaji wote wa DR Congo wakiongozwa na Henoc Inonga walikwenda kushangilia naye kwa staili yake ya kutetema.


Hata baada ya mechi ilikuwa ni staili ya Mayele waliyoitumia kushangilia nayo. DR Congo imejaza mastaa wanaocheza Ulaya, lakini staili ya ushangiliaji ya Mayele ndiyo inayovutia zaidi.


Haishangazi kuona mashabiki wanatetema hadi katika nyumba za Ibada. Nina uhakika wapo mashabiki wengi tu wa Yanga wanaoenda uwanjani sasa hivi kutetema na Mayele.


Unapompoteza Mayele unapoteza mambo mengi kwa pamoja kwani Mayele ni mshambuliaji wa aina gani kwako? Niandikie maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad