Dar es Salaam. Uraibu wa kamari na michezo ya kubeti, wadaiwa kuwa chanzo cha ugomvi uliosababisha mauaji ya Mwanahamisi Pauline (Mwana Mjeshi).
Dereva bajaj asimulia sakata mume aliyemuua mkewe kisha kujiua, ‘mke aliniomba nisimwambie mumewe’
Inadaiwa kuwa Omary Herman (39) maarufu kwa jina la Komi au Mjeshi, jana Jumatano Juni 28, 2023 alimuuwa mkewe ‘Mwana Mjeshi’ kwa kumchoma na kitu chenye ncha kali, na baadaye kujirusha kwenye treni iliyokuwa ikitoke Ubungo kwenda Gerezani, eneo la Ubungo Maziwa na hivyo kupoteza uhai wake.
Jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa kusema: “Taarifa hizo ni za kweli na yeye amejirusha kwenye treni, lakini tunaendelea kufuatilia kwa karibu, taarifa zaidi nitazitoa,” alisema Muliro.
Hata hivyo siku moja kabla ya kutekeleza tukio la mauaji hayo Komi aliandika jumbe mbili tofauti katika mtandao wa kijamii, wa Facebook zilizosema "Ndiyo imeshatokea na imebaki story" na nyingine "Yale maisha ya furaha yamekwisha sasa yamebaki ya huzuni".
Leo Juni 29, 2023; Mwananchi Digital ilifika msibani ambapo ilidaiwa kuwa wawili hao walikuwa na ugomvi wa muda mrefu kutokana na kile kilichoelezwa ni malalamiko ya mwanamke huyo kutokana na kitendo cha mumewe kucheza kamari, kubeti kiasi cha kushindwa kuihudumia familia.
Ally Godoro ambaye ni mjomba wa marehemu Mwanahamisi, ameiambia Mwananchi Digital kuwa wawili hao walikuwa na ugomvi wa ugomvi wa muda mrefu hadi kufikia hatua ya kwenda mkoani Morogoro kwa baba mzazi wa mwanamke kupata suluhisho la mgogoro wao.
"Mgogoro huu umekuwa wa muda mrefu na ulikuwa ukipelekwa kwa mzee kwa ajili ya kumaliza matatizo yao lakini haikusaidia hadi kufikia hatua ya kupeana talaka," alisema Godoro.
Naye dereva wa bajaji Imani Omary maarufu (Madega) ambaye alimsaidia marehemu Mwanahamisi kuhamisha vitu vyake siku moja kabla ya tukio la mauaji amesema, aliombwa na marehemu kumpeleka katika chumba kipya alichopanga na kuomba asimwambie mumewe Mjeshi mahali alipopanga.
"Mama Imani (marehemu) aliniomba nimbebee kitanda na godoro na alisema nisimwambie mumewe alipohamia, licha ya kuwa siku ya kuhamisha vitu vyake alisaidiwa na mumewe wake kubeba hadi barabarani," amesema Madega na kuongeza;
"Mwanamke alikuwa analalamika sana kuhusu tabia ya mumewe ya kuvuta bangi, kucheza kamari alimvumilia kwenye bangi lakini kwenye kubeti waligombana sababu pesa zote za mshahara ziliishia kwenye kubeti.”
Kwa upande wa Jeniffer Java, dada wa Komi; amesema taarifa za msiba wa wifi yao walizipata saa 2 asubuhi, na baadaye walienda eneo la tukio na kukuta mwili wake ukiwa chini umelala.
Hata hivyo licha ya kaka yao kutekeleza tukio hilo, waliweka vikao kwa ajili ya kujua namna ambavyo kama familia wangehusika katika msiba huo, na kwamba wakati wakiwa kwenye maandalizi hayo, alipokea taarifa ya msiba wa mdogo wake kuwa amejirusha kwenye treni.
"Majira ya saa 11 jioni tulipigiwa simu na msamaria mwema, kupitia simu ya wifi yetu (mwanamke aliyeuwawa) ambaye alituambia mwenye simu amefariki kwa kujirusha kwenye treni na kufa papo hapo," alisema na kuongeza;
"Tulipofika kwenye eneo la tukio mashuhuda walituambia, alikaa muda mrefu eneo lile na aliziweka simu zake pembeni, ilipokuja treni aliacha kichwa na behewa la kwanza na la pili lipite ndipo alipojirusha kwenye behewa la tatu," alisema Jenifer.
Jenifer ameliambia Mwananchi Digital kuwa: "Komi alikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na mkewe, sababu kubwa ni kubeti kwani pesa zote za mshahara zilikuwa zinaishia huko na mkewe hakuweza kuvumilia na kuamua kuomba talaka ili akanzishe maisha yake."
Aidha baada ya kuachana alisema marehemu (Mwanahamisi) alienda kwao Ngerengere, na alivyorudi Dar es Salaam alipanga chumba maeneo ya Gongo la Mboto na baadae kuamua kurudi Manzese kutokana na shughuli zake za ususi kuwa mbali na wateja wake.
"Wifi yetu ni msusi aliona kutoka Gongo la Mboto hadi Manzese ni mbali, alikuwa akitumia nauli nyingi akaamua kupanga jirani na shughuli zake, alivyopata chumba juzi na kuondoka alisaidiwa na mumewe, lakini jana (juzi) alimpigia simu mkewe aende kwake kuna mteja anahitaji kusuka na ndipo kulipotekeleza mauaji hayo," alisema na kuongeza.
Imeelezwa kuwa, wawili hao kabla ya kutengana; waliishi pamoja kwa miaka tisa, na kwamba wameacha watoto wawili Haiman Omary (7) na Abdulaziz Omary (2).
Mwananchi. Fikiri Tofauti.