Usipotupa majibu, hatupitishi bajeti yako – Musukuma



Usipotupa majibu, hatupitishi bajeti yako – Musukuma
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Musukuma’ amemcharukia Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza na kwamba asipokuwa na majibu mazuri wabunge wote wa Kanda ya Ziwa hawataunga mkono upitishwaji wa bajeti yake.

Akizungumza Bungeni leo Juni 23, 2023 Musukuma amesema kuwa kila mwaka kwa miaka saba mfululizo, serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa ndege wa Mwanza lakini haufanyiki.

“Najiuliza na bahati nzuri Mwigulu wewe ni mchumi, kila mwaka unatusomea matakwimu, unatupiga kanzu, tunasikia tu mabilioni ya kiwanja kipo hivi, vile jengo limejengwa kwa spidi limewekewa vioo mpaka vioo vinadondoka tumelogwa na nani?” alihoji na kuongeza

“Biashara ya ndege, ukiacha kiwanja cha Dar es Salaam kiwanja kingine kilichopo ‘busy’ ni cha Mwanza, tatizo ni nini, tunahitaji kuwa na kiwanja cha kimataifa cha Mwanza, mmenunua ndege kubwa ya mizigo, mnaitoa wapi mizigo kama kanda ya ziwa ndege haziendeki?


“Usipokuja na majibu mazuri ya kiwanja cha ndege cha Mwanza, wabunge wote wa Kanda ya Ziwa tutasimama na hatutakubaliana na wewe kupitisha bajeti yako, ishakuwa ‘to much’, ni dharau.

“Nikuombe jengo lipo ugomvi uliopo ni kati ya halmashauri na serikali, halmashauri ilitoa sh bilioni 2, serikali sijui irudishe, unatoaje hela kulia unaweka kushoto? chukua maamuzi tutengenezewe uwanja, tumechoka kupigwa swaga, mwaka wa saba kila mwaka tunawekewa bajeti ya uwanja alafu hivyo hivyo.;…… “haiwezekani, leo ndege zote za Tanzania biashara kubwa ipo Mwanza, mnaingiza pesa alafu sisi mnatuona mbayuwayu, hatutokubali.”Amesisitiza

Amesema, kutoka Mwanza kwenda Serengeti ni kilomita 90, hivyo wanataka kuona wazungu wanatua Mwanza wanaenda Serengeti.


“Hivi hamjiulizi matajiri wakubwa wanaokuja na jet hawaendi Kilimanjaro kwa vile ni mbali kilometa 500, wanatua Mwanza wanaacha jet wanapanda ndege dogo wanatua Serengeti kwa dakika 15 wanaona wanyama.

“Tumejenga mahoteli serikali mmejenga hoteli nzuri tu Capripointi lakini mmeitelekeza, mmeiacha tu imekuwa jumba la kulala popo kwa sababu hamna mkakati mzuri, nikuombe muheshimiwa Waziri (Mwigulu) ili kisiumane huko mbele unapokuja hapa utuambie uwanja wa ndege utajengwa lini, hatutapiga makofi hapa.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad