MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (CCM) amemtaka Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amuombe radhi Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa kwa kauli yake inayolenga kuchochea ubaguzi.
Mwita ametoa kauli hiyo leo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia makubaliano ya awali kuhusu mapendekezo ya kuridhia mkataba baina ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai katika ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uendelezaji na uboreshaji wa utendaji kazi wa bandari za Tanzania.
“Ningekubaliana na ndugu yangu (Mbowe) kama angekosoa vifungu kwenye makubaliano hayo, lakini kitendo cha kusema rais mzanzibar anauza bandari na Mbarawa ni mzanzibar anauza mali ya Tanganyika, amemkosea sana rais, Mbarawa na watanzania… anapaswa kuomba radhi kwani hii dalili mbaya za kutaka kuligawa Taifa hili,” amesema.
Wito huo wa Waitara umekuja siku chache baada ya Mbowe kujadili mkataba huo na kudai kwamba “Wakati mkataba umetiwa saini na Waziri Makame Mnyaa Mbarawa, Mzanzibari, kwa mamlaka aliyokasimiwa na Rais Samia Suluh Hassan, Mzanzibari pia, mkataba wenyewe unahusu bandari zote zilizopo upande wa Tanganyika peke yake,”
Aidha, Waitara ametoa rai kwa wabunge kuunga mkono makubaliano hayo yaliyowasilishwa bungeni na Prof. Mbarawa kwa kuwa anaamini Rais Samia pamoja na Spika Tulia Ackson ambaye ni mbobevu wa sharia hawezi kuruhusu makubaliano mabovu yaingizwe bungeni.
Waitara alienda mbali na kuwahoji wabunge kama kuna yeyote aliyewahi kuuona mkataba wa miradi mikubwa kama ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa daraja za Tanzanite – Dar es Salaam na Kigogo Busisi Mwanza au mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Baada ya wabunge kukiri hawajahi kuina mikataba ya miradi hiyo ya kimkakati, Waitara alisema limekuwa jambo la kipekee kwa mkataba huo wa makubaliano kati ya Serikali Tanzania na Dubai kuwekwa wazi kiasi hicho hivyo inaonesha namna Rais Samia anavyopendelea uwazi na ukweli.