Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kwamba Serikali haitodharau maoni na ushauri wanaoutoa kuhusu maeneo yenye hofu kwenye mradi wa uwekezaji wa Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Majaliwa amewataka pia Watanzania waendelee kuwa na imani na Serikali pamoja na wawakilishi wao ndani ya Bunge kwani Serikali imejidhatiti kuhakikisha bandari inakuwa na ufanisi unaoendana na mahitaji ya sasa na kwa kuzingatia manufaa ya kijiografia ya Nchi yetu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumanne, Juni 20, 2023 katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 40 ya chuo cha International Evangelism Centre kilichoko Sakila jijini Arusha ambapo amesema bandari haijauzwa, bali Serikali inataka kubadilisha Muwekezaji ili iweze kuendeshwa kwa ufanisi na tija zaidi.
Majaliwa amesema wakati wa kuingia mikataba utakapofika Wataalamu wa uchumi nchini wataishauri Serikali kuhusu muda wa uendeshaji wa uwekezaji huo, hivyo amewataka Wananchi waendelee kuwa na subra.